
SI mmeona jamani, Mwarabu amelowa nyumbani kwake! Hicho ndicho ilichokifanya Yanga SC jana Jumatano pale Tunis nchini Tunisia kwa kuibuka na ushindi wa bao 0-1 dhidi ya Club Africain na kufuzu kibabe hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga ambayo ilikwenda kwenye mchezo huo kwa lengo la kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kufeli Ligi ya Mabingwa Afrika, hatimaye imefanikiwa kwa ushindi wa jumla ya bao 1-0 baada ya mchezo wa kwanza nyumbani matokeo kuwa 0-0.
Bao la Stephane Aziz Ki dakika ya 79 akiunganisha pasi ya Fiston Mayele, lilitosha kuipa Yanga ushindi huo muhimu ambao ilikuwa ikiuhitaji kwa muda mrefu.

Aziz Ki ndiye aliiteka shoo kwani kuingia kwake kipindi cha pili akichukua nafasi ya Khalid Aucho, kulibadilisha mchezo kwa kiasi kikubwa hadi kupatikana ushindi huo.
Kitendo cha Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, imekuja baada ya mara ya mwisho kucheza hatua ya hiyo mwaka 2018.
Kabla ya mchezo huo wa jana, Club Africain ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda kutokana na msimu huu kuwa na rekodi nzuri nyumbani katika michuano ya kimataifa ikitoka kuichakaza Kipanga FC ya Zanzibar mabao 7-0.