
MAHAKAMA ya Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, katika kesi yake ya kwanza kuitolea hukumu tangu izinduliwe Novemba 25, 2022 na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahimu Juma, imewahukumu watu wawili ambao ni mama na mtoto wake kutumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja baada ya kukiri kosa katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa inawakabili.
Kesi hiyo ya kwanza ya uhujumu uchumi kusajiliwa na kutolewa hukumu kwenye mahakama hiyo, lakini pia imeendeshwa kwa muda mfupi wa saa moja na kutolewa hukumu baada ya washtakiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kukiri kosa.
Kija Matu (60) na Mayunga Juma (30) ndiyo waliokumbana na adhabu hiyo baada ya kukiri kosa la kukutwa na nyara za serikali ambazo ni vipande 8 vikavu vya mnyama aina ya nyumbu kinyume cha sheria vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 1,517,100.
Katika kesi No. 1 ya mwaka 2022 ya uhujumu uchumi, kabla ya hukumu hiyo washtakiwa walisomewa mashtaka yao na Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka ofisi ya mashtaka, Jaston Haule.
Jaston alielezea mahakama kuwa washtakiwa wote wawili mnamo Desemba 5, 2022 majira ya saa 4:00 usiku katika Kijiji cha Laini ‘B’ wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu, walikamatwa na kufanyiwa upekuzi ambapo walikutwa na vipande hivyo 8 vikavu vya nyumbu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote wawili walikiri kosa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Robert Kaanmwa aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, alitoa adhabu ya kwenda jela kwa kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20.