
Asubuhi ya leo, taharuki kubwa imeibuka kwenye mitandao ya kijamii, ikieleza kwamba watu 10 wamepoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa baada ya Ndege aina ya Garet 5Q KTM ikiwa na abiria 42, ikidaiwa kutokea nchini Rwanda kuelekea Msumbiji kupitia Dar es Salaam kuanguka nje kidogo ya uwanja wa ndege wa Kahama wakati ikijaribu kutua kwa dharura kwenye uwanja huo.
Habari hizo, zikazidi kushibishwa na video ya Meneja wa Uwanja wa Kahama, Hamza Kyemo, kusambaa ikitoa ufafanuzi kuhusu ajali hiyo.

Hata hivyo, baadaye imekuja kubainika kwamba, hakuna ajali iliyotokea isipokuwa lilikuwa ni zoezi la kupima utayari, lililolihusisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na wafanyakazi wa uwanja huo wa ndege.
Baada ya ufafanuzi huo uliotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita kwamba siyo ajali bali ni mazoezi ya utayari, umemaliza taharuki kubwa iliyokuwa imetanda ndani na nje ya nchi.