×

Simba Yazindua Tena Kadi ya Shabiki – Video

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.

UONGOZI wa KIabu ya Simba kwa ushirikiano na Benki ya Equity umefanya uzinduzi wa pili wa kadi ya shabiki uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar.

 

Uzinduzi huo ni wa pili baada ya ule wa kwanza uliofanyika katika Viwanja vya Sabasaba uliohudhuriwa na viongozi wa Equity na wale wa Simba.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema kuwa uzinduzi huo ambao utakuwa endelevu una lengo la kuifanya klabu hiyo kuendeshwa kisasa zaidi pamoja na kuwapa fursa za huduma mbalimbali mashabiki wa klabu hiyo kongwe nchini.

 

“Sisi kama Simba tumeazimia kuifanya kwa vitendo kauli yetu ya ‘This is next level’ kwa kuileta kadi hii ya mashabiki ambayo inakuja na faida mbalimbali kwa klabu na wanachama kama ifuatavyo.

 

“Kwanza ni katika kuisaidia klabu kujiendesha kisasa zaidi kutokana na mapato yatakayokuwa yanapatikana kwa kuichangia kadi hii kwani katika elfu 22 ambayo mwanachama atalipia kiasi cha shilingi elfu 12 kitaingia katika klabu yetu kwa ajili ya maendeleo ya klabu ambayo kwa wanachama laki moja unapata kiasi cha shilingi bilioni moja na zaidi.

 

“Pili kwa shabiki atakayelipia kadi hii atapata nafasi ya moja kwa moja kujiunga na kuwa na akaunti katika Benki ya Equity, akaunti ambayo haina makato ya mwezi, akaunti hii pia itamwezesha shabiki kufanya miamala ya kulipia huduma mbalimbali kupitia simu yake ya mkononi sambamba na hayo shabiki pia atakuwa na haki ya kupata kadi ya uanachama ambayo huwezi kuwa nayo pasipokuwa na kadi ya shabiki.

 

“Pia tunataka kutangaza kuwa Jumatano ya tarehe 29 tutakuwa na uzinduzi wa tatu katika Kanda ya Kati ambapo Spika wa Bunge, Mhe Job Ndugai atazindua tukio hilo la kwanza na la pekee pamoja na lile la kuzindua Tawi la Simba Bungeni litakalojulikana kama Simba mjengoni,” alisema Manara.

 

Pamoja na hayo pia Mkurugenzi wa Mashabiki wa Simba na Project Manager wa Equity walikazia suala la umuhimu wa mashabiki kuwa na kadi hizi.

Leave a Comment