×

Wanafunzi Watatu Wauawa Kwa Kupigwa Risasi, Wengine Watano Wajeruhiwa

 

Watu watatu wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa baada ya mwanaume mwenye silaha kuvamia Chuo Kikuu cha Michigan, Marekani usiku wa jana Jumatatu, Februari 13, 2023 na kuanza kufyatua risasi akiwalenga wanafunzi wa chuo hicho.

 

Polisi wameeleza kwamba muda mfupi baada ya tukio hilo, walimkuta mwanaume aliyekuwa akifyatua risasi, naye akiwa amekufa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kujipiga risasi.

 

 

 

Inaelezwa kwamba baada ya kufanikiwa kuingia kwenye chuo hicho, mwanaume huyo akiwa na bunduki, alianzia kufanya mashambulizi katika Ukumbi wa Berkey Hall wa chuo hicho, kisha akahamia katika eneo la MSU Union ambalo hutumika na wanafunzi wa chuo hicho kwa kula na kujisomea.

 

Kaimu Mkuu wa Polisi wa Michigan, Chris Rozman amenukuliwa asubuhi ya leo, Jumanne April 14, 2023 akieleza kwamba hakuna tena tishio kwenye chuo hicho na wameongeza ulinzi katika maeneo yote ya chuo na kwamba mwanaume aliyetekeleza tukio hilo, alifanya mwenyewe bila kushirikiana na mtu yeyote.

Wanafunzi wakiwa na taharuki.

 

Rozman ameeleza kwamba walipokea simu ya kwanza kutoka chuoni hapo majira ya saa 2:18 usiku ikitoa taarifa kuhusu mtu aliyekuwa akifyatua risasi katika Ukumbi wa Berkey ndani ya chuo hicho ambapo ndani ya muda mfupi, polisi walifika eneo hilo lakini tayari mtuhumiwa alikuwa ameshasababisha maafa hayo.

 

Mtuhumiwa akiingia ndani ya eneo la chuo hicho.

 

Ameeleza kwamba baada ya kufika chuoni hapo, walikuta wanafunzi wakiwa kwenye taharuki kubwa ambapo walitoa huduma ya kwanza kwa majeruhi ambao walikimbizwa katika Hospitali ya E.W. Sparrow kwa matibabu.

 

Bado mtuhumiwa wa tukio hilo, hajatambuliwa na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu sababu zilizomfanya mwanaume huyo kutekeleza mauaji hayo kisha kujipiga risasi.

Leave a Comment