×

CTI Yaomba Malighafi Zinazoingia Tanzania Zisitozwe Kodi

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba akizungumza wakati wa mkutano na wanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI). Anayefuata ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashaar, Dk. Ashatu Kijaji na Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza.

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda Nchini (CTI), limeiomba serikali kupunguza au kuondoa  kodi kwa malighafi zinazotoka nje ya nchi kwaajili ya kusaidia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali hapa nchini na kuzitoza kodi stahiki zile bidhaa zinazotoka nje ya nchi.

Hayo yamesemwa jinini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa (CTI), Leodeger Tenga, wakati wa kikao baina ya shirikisho hilo na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba.

Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodeger Tenga akizungumza na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba walipofika kuzungumza na wafanyabiashara na wenye viwanda leo

“Lazima tuwe waangalifu sana kwa viwanda vyetu vya ndani, unaposema soko huru unaweza kukuta wewe unageuzwa soko la bidhaa za wenzako kama hukutengeneza mazingira mazuri kwa watu wako wa ndani kuzalisha bidhaa nzuri na kwa bei nafuu,” alisema

Alisema mkutano umekuwa na manufaa makubwa kutokana na wafanyabiashara hao kupata fursa ya kuelezea yanayowakwaza kutoka kwa mawaziri wawili kuhusu mazingira ya biashara.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuhakikisha kwamba wanajenga mazingira wezeshi ya ufanyaji mzuri wa biashara unaovutia uwekezaji na wawekezaji wanapokuja wakute mazingira mazuri.

Wenye viwanda waliohudhuria mkutano huo wakijadiliana jambo.

“Pia imekuwa nafasi nzuri kwa wenye viwanda na wafanyabiashara kuishukuru serikali kwa mambo mema ambayo imefanya ambayo yako mengi na pia kukumbushana mengine ambayo bado yanahitaji kufanyiwa kazi,” alisema

Alisema changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili wafanyabiashara zimefanyiwa kazi na serikali lakini aliomba kero ziliozosalia zifanyiwe kazi kwa haraka ili kuvutia uwekezaji kwa wingi kutoka nje.

Aliwataka wazalishaji wa Tanzania kujitahidi kuzalisha bidhaa bora na zenye unafuu ili ziweze kuvutia masoko mengi na makubwa kwa Afrika Mashariki na kwingineko duniani.

“Kama nchi imeshafanya maamuzi ya msingi ya kuingia kwenye soko huru la Afrika na tuko pia kwenye soko la Afrika Mashariki hivyo ili tuweze kushindana lazima tuzalishe bidhaa bora vinginevyo tutageuka soko la wenzetu kwa hiyo hakuna namna lazima tuzalishe bidhaa bora ili tushindane,” alisema.

Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza akizungumza kwenye mkutano huo

“Lazima tushindane kwa mambo mawili, tushindane kwa ubora na tushindane kwa bei. Wakati mwingine bidhaa zinaongezeka bei kutokana na changamoto za usafiri au za kikodi sasa yale ya kikodi tayari mapendelezo yetu ya kikodi yameshawasilishwa serikalini,” alisema

Wakati huo huo, Serikali imetangaza kuwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu itaanza kupeleka aina 10 za bidhaa  katika Soko la Huru la Biashara Afrika  ambalo Tanzania ni mwanachama.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi saba za mwanzo zilizopewa kipaumbele cha kupeleka bidhaa kwenye soko hilo hivyo kuwataka wafanyabiashara wachangamkie fursa hiyo adimu.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba akizungumza kwenye mkutano huo

“Tumeshakutana Januari na leo ni kikao chetu cha tatu kukutana na wadau wazalishaji wa viwanda na wafanyabiashara kuelimishana kuhusu kinachohitajika kwenye eneo huru la biashara Afrika,” alisema

“Tayari tumeshapata bidhaa ya kwanza itakayotangulia ambayo ni kahawa na hatutapeleka ikiwa ghafi tutapeleka iliyokwishachakatwa (finished product),” alisema Waziri Kijaji

Alitaja bidhaa nyingine itakayopelekwa kwenye soko hilo kuwa ni marumaru zinazozalishwa hapa nchini na kwamba serikali imeshajadiliana na wazalishaji wa bidhaa hiyo na wako tayari kusafirisha.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia mkutano huo uliofanyika leo hoteli ya New Afrika

“Kuna bidhaa zingine bado tunajadiliana na wazalishaji sitaziweka wazi leo lakini kwa ujumla tuko tayari kuingia na aina 10 za bidhaa kwenye soko hili kuanzia Julai Mosi mwaka huu tunaendelea kuelezana kinachohitajika na vitu vya kuzingatia kutoka kwa wazalishaji wetu wa ndani,” alisema

“Niwahakikishie wazalishaji wetu wa viwandani na wale wa bidhaa zingine kwamba serikali iko tayari na vikao hivi ni endelevu tutaendela kupeana taarifa na kama alivyosema mheshimiwa Rais kwamba tusiwe wasindikizaji kwenye hili soko,”alisema

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, akipokelewa na viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), alipokwenda kuzungumza na wenye viwanda na wafanyabiashara kusikiliza kero zao na kuzijibu

Leave a Comment