
MSHAMBULIAJI wa Simba, Moses Phiri, amesema licha ya matokeo mabaya ambayo wameyapata mfululizo, lakini wao kama wachezaji bado hawajakata tamaa kwa ajili ya kuipigania timu hiyo kufanya vizuri.
Simba imeshindwa kupata ushindi katika michezo mitatu iliyopita ya michuano yote ambapo imepoteza miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya na Raja Casablanca, kisha wakapata sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC.
Akizungumza na Spoti Xtra, Phiri alisema wao kama wachezaji bado hawajakata tamaa na wanaamini hiki ni kipindi cha mpito kwani watarejea katika ubora wao na kupata matokeo mazuri ya kuwapendeza Wanasimba wote.
“Kwenye mpira hiyo ipo, lakini najua ni ngumu kwa mashabiki kuvumilia haya kwa kuwa wanaumizwa na matokeo wakiwa wanatamani kufurahi katika kila mchezo.
“Sisi wachezaji tunafahamu na tunawaahidi mashabiki wetu kuwa tutapambana katika michezo ijayo tuweze kupata matokeo mazuri mara baada ya kushindwa kupata matokeo hayo katika michezo mitatu iliyopita, mashabiki watafurahi kwani na sisi hatupendezwi na matokeo haya,” alisema mchezaji huyo.
STORI NA MARCO MZUMBE