Saa kadhaa baada ya kifo cha msanii Constantinos Tsobanoglou (Sobanoglu) almaarufu Costa Titch aliyeanguka ghafla jukwaani akiwa kwenye shoo na kupoteza maisha usiku wa kuamkia leo, Machi 12, 2023, imetoa tamko na kuthibitisha kifo cha msanii huyo.
Katika taarifa iliyotumwa kupitia akaunti ya Costa Titch katika mtandao wa kijamii wa Instagram, familia yake imeeleza kuwa imepokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha mpendwa wao aliyefikwa na umauti akiwa na umri wa miaka 28.
“Tunawashukuru watoa huduma ya kwanza na dharura na wote walioshiriki kujaribu kuokoa maisha ya mpendwa wetu. Kama familia tupo kwenye wakati mgumu cha kutafakari kifo cha ghafla cha mpendwa wetu na tunaomba muda na nafasi wakati tukiendelea kutafakari nini cha kufanya,” imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa imeendelea kueleza kuwa familia hiyo inawashukuru watu wote waliokuwa wakimpa sapoti mpendwa wao katika kazi yake ya muziki enzi za uhai wake, na kuwaomba waendelee kumuombea apate pumziko la Amani.