
MABOSI wa Yanga wapo katika mazungumzo ya mwisho na beki wa kati wa timu hiyo, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kwa ajili ya kumuongezea mkataba mpya wa kuendelea kukipiga kikosini hapo.
Beki huyo alijiunga na Yanga dirisha dogo la msimu uliopita akitokea KMKM ya Zanzibar akisaini mkataba wa miaka miwili.
Yanga ilimsaijili Bacca baada ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia, Nasreddine Nabi kuvutiwa na kiwango alichokionesha katika Kombe la Mapinduzi 2022.

Akizungumza na Spoti Xtra, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alisema muda wowote beki huyo atasaini mkataba mwingine wa miaka miwili kwani hivi sasa wapo kwenye mazungumzo.
Said alisema maboresho makubwa watayafanya katika mkataba wake huo mpya na kuongeza kwamba, sababu ya kumuongezea mkataba huo ni kutokana na ubora na kiwango kizuri anachoendelea kukionesha uwanjani.
“Bacca ana vigezo vyote vya kuwa beki bora, ana uwezo wa kucheza mipira ya juu na chini na mzuri zaidi katika ‘tackling’, hivyo anastaili kuongezewa mkataba mwingine.
“Ni kawaida kwa Yanga kuona inaboresha mikataba ya wachezaji wake wale waliokuwepo katika kiwango bora, tangu Bacca ameingia katika kikosi cha kwanza, ameonesha ni mchezaji mzuri,” alisema Said.
STORI NA WILBERT MOLANDI