×

Hizi Hapa Mashine 5 Za Kuwaua Marumo Mchezo wa Marudiano Afrika Kusini

KUELEKEA mchezo wao wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa kesho Jumatano dhidi ya Marumo Gallants nchini Afrika Kusini, mapema tu Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amemaliza hesabu baada ya kuwaandaa nyota wake watano kwa ajili ya kuumaliza mchezo huo wa marudiano.

Ishu nzima iko hivi, Yanga Jumamosi ilikuwa na mchezo muhimu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar ambapo Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 4-2 na kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo huku wakiwa wamesaliwa na michezo miwili.

Katika mchezo huo dhidi ya Dodoma Jiji, kocha wa Yanga aliwapumzisha wachezaji watano ambao walianza katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza dhidi ya Marumo Galllants iliyopigwa jijini Dar ambayo Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Wachezaji ambao walianza kwenye nusu fainali ya kwanza na Marumo ambao hawakuwa sehemu ya mchezo wa juzi Jumamosi dhidi ya Dodoma Jiji ni Djigui Diarra, Khalid Aucho, Dickson Job, Ibrahim Bacca na nahodha Bakari Mwamnyeto.

Akizungumza na Championi Jumatatu, kuhusiana na mabadiliko ya kikosi chake kuelekea mchezo dhidi ya Marumo, Nabi alisema: “Tumekuwa na ratiba ya michezo mingi migumu ambayo imefuatana, hivyo ili kupunguza majeraha na kuhakikisha tunakuwa na wachezaji ambao wana utimamu sahihi wa miili tulilazimika kufanya mabadiliko hayo ya lazima.”

Stori na Joel Thomas

Leave a Comment