
MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara Yanga Sc wameendeleza wimbi la ushindi baada ya leo Desemba 19 kufanikiwa kuchukua alama tatu mbele ya Dodoma Jiji, wakishinda kwa mbao 3-1, mechi hiyo imechezwa katika dimba la Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.
Dodoma Jiji walianza mechi hiyo kwa kasi na kufanikiwa kupachika bao la mapema baada ya mlinda mlango wa Yanga, Metacha Mnata kufanya uzembe kwenye lango lake na kumpa nafasi Seif Karihe kuandika goli la kuongoza dakika ya 3 ya mchezo.
Baada ya Goli hilo timu ya wananchi walionekana kuzinduka na kuanza kulisakama lango la Dodoma Jiji na kufanikiwa kusawazisha goli hilo kupitia kwa beki na nahodha wa kikosi hicho Lamine Moro dakika ya 27 ya mchezo.

Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko Michael Sarpong alienda benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyefunga goli matata la mkwaju wa adhabu dakika ya 68, hii ikiwa ni mechi ya kwanza kwenye ligi, zikiwa zimepita siku chache tangu afunge kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Singida United.
Beki kitasa, Bakari Mwamnyeto alihitimisha ushindi kwa Yanga kwa kufunga bao dakika ya 75, kwa matokeo hayo sasa Yanga wanaongoza ligi kwa pointi 40, huku safu ya ushambuliaji ikionekana kuimarika chini ya kocha Cedric Kaze.