×

Airtel Wachangia Damu Kuunga Mkono Juhudi za Serikali Kuboresha Huduma za Afya.

Meneja Rasimaliwatu wa Airtel Tanzania Jacqueline Lyakurwa akishiriki zoezi la kuchangia damu kwa wahitaji wa damu kupitia benki ya damu salama. Zoezi la uchangiaji damu kwa hiari lilifanyika makao makuu ya Airtel Moroco jijini Dar es salaam kwa lengo la kusaidia kuokoa maisha ya wahitaji damu.

Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Uchangiaji Damu nchini (NBTS) Leo wameungana na wachangia damu wengine kwa kuchangia damu kwa hiari ili kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha afya nchini. Siku ya Damu Salama ni siku ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO) hiutumia kuhamasisha afya salama. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ’Give blood, give plasma, share life, share often’ Hii inadhihirisha umuhimu wa kila mtu kujitoa kwa zawadi ya kipekee kwa  kuchangia damu na kuoakoa Maisha ya wahitaji,

Akizungumza Leo jijini Dar es Salaam wakati wa zoezi la kuchangia damu lililofanyika makao makuu ya kampuni ya Airtel, Mkurugenzi Rasimaliwatu Airtel Bi Stella Kibacha alisema kuwa kuchangia damu ni jambo muhimu kwani kunasaidia kuokoa maisha ya wenye uhitaji. Tunatambua ya kwamba damu inahitajika sana Hospitali na hasa pale wakina mama wanapokuwa wanajifungua, vile vile kwa watoto wenye magonjwa mbali mbali kama malaria, majeruhi wa ajali, wagonjwa wa kansa pamoja na wagonjwa wengine.

Wafanyakazi wa Airtel pichani wakishiriki zoezi la uchangiaji damu kwa hiari kupitia benki ya damu salama. Zoezi la uchangiaji damu kwa hiari lilifanyika makao makuu ya Airtel Moroco jijini Dar es salaam ili kusaidia kuokoa maisha ya wahitaji damu nchini.

‘Kwa sababu hiyo, sisi wafanyakazi wa Airtel tumeamua kuchangia damu na pia tukio hili liwe hamasa kwa wananchi wengine kijitokeza na kuchangia damu’ alisema Kibacha.

 Msimamizi wa zoezi la Uchangiaji damu wa Kanda ya Kati Fatma Majungu alisema, Benki ya damu salama hapa nchini inahitaji kiasi cha uniti za damu 600,000 za damu kwa mwaka kwa ajili ya huduma za dharura na matumizi mengine ya afya, lakini makusanyo ya Damu kwa mwaka jana ni asilimia 65  ya mahitaji yetu.

“Upatikanaji wa damu bado ni changamoto. Taarifa ya mwaka 2019/2020 ya ukusanyaji wa damu nchini inaonyesha kuwa asilimia 60 ya waliochangia damu walifanya hivyo kwa hiari yao na kati yao ni asilimia 8 tu hufanya hivyo mara kwa mara. Bado tunahimiza wachangiaji kuendelea kuchangia kutokana na uhitaji wa damu tulionao. Alieleza Fatma

“Naniwapongeza Watanzania pamoja na wafanyakazi wa Airtel kwa kujitokeza kushiriki kwenye zoezi hili la kuchangia damu kwa mwaka huu na niwaombe waendelee hivyo ili kuendelea kuokoa maisha ya wengine” aliongeza Fatma.

 

Siku ya kuchangia damu unaadhimisha Juni 14 kila mwaka. Siku hii ni maalum kukumbuka na kutambua umuhimu wa damu salama. Pia ni siku ya kusherekea na kuwakumbuka wale wote wanaochangia damu kwa hiari

 

Leave a Comment