×

Yanga: Kocha Anayekuja Atatikisa Nchi… Kocha Jozef Vukusic Atajwa Kutua

Mtunisia Nasreddine Nabi

KAMATI ya Utendaji na Mashindano ya Yanga jana usiku ilitarajiwa kukutana kwa ajili ya kuanza mchakato wa kumpata mrithi wa aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia Nasreddine Nabi huku jina la Jozef Vukusic likitajwa kwa ukaribu kurithi mikoba yake.

Hiyo ikiwa ni saa chache tangu Yanga itangaze kuachana na kocha huyo aliyeipa mafanikio makubwa katika msimu huu ikiwemo kuifikisha timu hiyo, katika hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

MAKOCHA WANOTAJWA

Hadi sasa kuna makocha kadhaa wanatajwa kulengwa na Yanga kuwa mbioni kuchukua mikoba ya Nabi ambaye ameondoka kikosini hapo akiwemo Jozef Vukusic raia wa Slovakia mwenye miaka 48.

Kocha huyo anahusudu mfumo wa 4-3-3 na amewahi kuzifundisha klabu mbalimbali ikiwemo AmaZulu FC, Polokwane City zote za Afrika Kusini, Ruzomberok ya nchini mwake na nyingi kibao.

Kocha mwingine anayetajwa ni Kocha wa Al Hilal ya Sudan, Mkongomani Florent Ibenge ambaye pia anatajwa kutakiwa na Primeiro de Agosto ya nchini Angola.

VIONGOZI WAKO KWENYE MCHAKATO

Championi Ijumaa, linafahamu kuwa tayari uongozi wa timu hiyo, umeanza mazungumzo ya haraka na baadhi ya makocha watakaokuja kuanza pre season kuelekea msimu ujao.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa baadhi ya majina yanatarajiwa kuwekwa mezani watakapokutana kwa ajili ya kupitia CV zao huku sifa kubwa anayotakiwa awe nayo ni kocha huyo kuifikisha Yanga katika hatua ya fainali ya michuano ya kimataifa Afrika.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe

Aliongeza kuwa uongozi huo umepanga kumpata kocha huyo hadi kufikia wiki ijayo, kwa lengo la kuanza mapema ya kuanza mapema maandalizi ya msimu ujao ambao malengo yao kufanya vema zaidi kimataifa.

“Wanayanga waondoe hofu, kama alikuja kocha bora kama Nabi na kuifanyia makubwa Yanga ikiwemo kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, basi ndivyo atakvyokuja kocha mpya mwengine.

“Tumepanga kumleta kocha mwingine mwenye CV kubwa ya michuano ya kimataifa, na lengo kubwa ni kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

“Kikao cha leo (jana) usiku tutakachokaa ndio kitatoa picha halisi ya kocha gani atakayekuja kumrithi Nabi, tumetoa nafasi za baadhi ya makocha kuwasilisha CV zao kwa ajili ya kuzipitia,” alisema mtoa taarifa huyo.

Akizungumzia hilo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe jana alisema kuwa: “Mchakato wa kumpata kocha mpya unafanywa kwa utaratibu ili kuhakikisha wanaendeleza kazi kubwa iliyofanywa na Nabi.

“Katika maombi yaliyotumwa wako makocha wakubwa kwelikweli, hii ni klabu kubwa na makocha wakubwa wanataka kuja kufanya kazi  Yanga.

Jozef Vukusic.

“Uongozi uliomleta Nabi Yanga ndio utakaomshusha kocha mkubwa atakayeitikisa nchi, atakuja kuongeza thamani kwenye nchi yetu na kuongeza mafanikio makubwa kwenye michuano ya ndani na ya kimataifa.”

KUHUSU MAKOCHA WENGINE

Kamwe alisema: “Wako watu ambao mikataba imeisha sio tu wa benchi la ufundi pia wachezaji kwa sasa tuko kwenye tathmini kulingana na ‘pafomansi’ yake kwa kuangalia kipindi wakati tunampa mkataba.”

INJINIA HERSI ASHUSHA PRESHA

Rais wa Yanga Injinia Hersi Said jana alitoa kauli ya matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo, pamoja na kumtakia kila la heri kwa kusema kuwa: “Kila la heri kocha Nabi, lakini niwahakikishie Wananchi kuwa, furaha tulionayo itaendelea Jangwani, tuwe watulivu katika kipindi hichi.”

STORI NA WILBERT MOLANDI

SALEH JEMBE ATEMA CHECHE BAADA ya SIMBA KUINGIA MKATABA wa BILIONI 2 “NILIGOMBANA na MENEJA wa TIMU”

Leave a Comment