
BAADA ya Kocha Nassredine Nabi kuondoka baada ya kumaliza mkataba wake Yanga, sasa ni zamu ya kiungo mkabaji, Yannick Bangala ambaye inaelezwa kuwa yupo mbioni kuondoka kwenda katika timu hiyo.
Kocha Nabi anatajwa kwenda kujiunga na klabu ya Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini mara baada ya kumaliza mkataba wake Yanga.
Chanzo cha kuaminika ambacho ni rafiki wa Bangala kutoka DR Congo kimeliambia Championi Ijumaa kuwa, kiungo huyo ana ofa nyingi mezani kwake na baadhi ya klabu zimeonyesha wazi kuwa tayari kuvunja mkataba ndani ya Yanga na kumbeba kiungo huyo ambaye ni mchezji bora wa ligi kuu msimu uliopita.
Kiliongeza kuwa, kati ya ofa hizo kuna klabu moja kutoka Tanzania na nyingine ni za nje ya nchi hivyo uwezekano wa kubaki Yanga ni 20% pekee na 80% ni za kuondoka.
“Bangala ana ofa nyingi sana ambazo zipo mbele yake, katika ofa hizo zote kuna timu kubwa sana ambazo zimeonyesha nia ya kweli ya kuhakikisha kuwa wanampata mchezaji huyo ambaye ni mmoja kati ya wachezaji walioonyesha mafanikio makubwa ndani ya Yanga.
“Bangala mwenyewe yupo tayari kuondoka ndani ya Yanga kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika michezo ya mwisho na yeye mwenyewe yupo tayari kwenda kutafuta changamoto mpya mara baada ya kufanya vyema akiwa na Yanga kwa kuipatia makombe yote muhimu,” kilisema Chanzo hiko.
Alipotafutwa Bangala ili azungumzie ishu hii alisema: “Ni kweli mimi nina ofa kubwa kutoka nje ya Tanzania na timu nyingine kubwa kutoka hapahapa Tanzania zimeonyesha nia ya kunitaka, kwangu nimebakiza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuichezea Yanga hivyo niseme kuwa nina asilimia 20 za kubaki Yanga na nina asilimia 80 za kuondoka.”
Stori na Marco Mzumbe