
Pwani, 18 Juni 2023: TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere imeungwa mkono kwa kuhamasisha watu kujitolea damu kusaidia wagonjwa ambapo chupa 35 zimepatikana katika zoezi hilo.
Hayo yalisemwa katika katika Zahanati ya Mlandizi na Yahaya Mbungulume ambaye alimwakilisha Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha baada ya zoezi la uchangiaji damu lililofanywa kwa pamoja na Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kushirikiana na Taasisi ya Chawa wa Mama Kibaha Vijijini ambapo watu binafsi wametakiwa kujitokeza kuchangia damu ili kunusuru wagonjwa wanaohitaji damu kwani ni muhimu katika kuokoa maisha ya watu.
Mbungulume alisema kuwa damu huwa haitoshi na inahitajika muda wote kwa ajili ya wagonjwa wakiwemo wajawazito, wagonjwa wa ajali na wagonjwa wa kawaida wanaohudumiwa kwenye Hospitali mbalimbali nchini.

Alisema damu ni sehemu muhimu ya tiba kwa wagonjwa amewataka Watanzania kujitolea kuchangia damu.
Kwa upande wake katibu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere mkoa wa Pwani, Omary Pumzi alisema kuwa waliamua kujitolea damu baada ya kupita kwenye Hospitali na kuona jinsi gani kuna uhitaji mkubwa wa damu.
Pumzi amesema kuwa taasisi hiyo imeendelea kutekeleza malengo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya kukabiliana na adui wa maendeleo ambao ni maradhi ujinga na umaskini hivyo afya ni moja ya malengo kama ilivyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.
Akiongoza zoezi la uchangiaji damu Katibu Msaidizi wa Taasisi ya Mwalimu Taifa Neema Mkwachu alisema wanamuunga mkono Mwasisi wa Taifa kwa vitendo kwa kushiriki moja kwa moja.
Akielezea mafanikio ya zoezi la uchangiaji damu mratibu wa huduma za maabara Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Nabwike Mwairinga alisema kuwa wamepata ‘unit’ 32 kwenye zoezi hilo ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kwenye benki ya damu ambapo wanahitaji unit 40 kwa kila mwezi.