×

Makampuni Kuwania Tuzo Zaidi Ya 70 Kwenye Consumer Choice Awards Afrika 2023

Mwanzilishi wa tuzo za Consumer Choice Awards Africa(CCAA) Diana Laizer, akiongea wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo kwa mwaka 2023. Hafla ya uzinduzi ilifanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau pamoja na wadhamini wa tuzo hizo.

Dar es Salaam 18, Juni 2023. Ikiwa ni sehemu ya kusaidia walaji kutoa maoni yao juu ya ubora wa bidhaa na huduma wanazozipata sokoni, tuzo za Consumer Choice Awards Africa (CCAA) mwaka huu zinatarajia kushindanisha makampuni mbalimbali katika aina zaidi ya 70 za tuzo.

Akizungumza katika uzinduzi wa tuzo za mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa CCAA Diana Laizer alisema mashindano ya mwaka huu yatahusisha aina kuu 22 za tuzo pamoja na nyingine ndogondogo zaidi ya 70.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Latifa Khamis akiongea kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji , Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaju wakati wa uzinduzi wa tuzo za Consumer Choice Awards Africa(CCAA) jijini Dar es Salaam.

Alitaja aina za tuzo zitakazoshindaniwa kuwa ni pamoja na Usafirishaji, Mawasiliano ya simu, Usafiri wa Anga, Huduma za kifedha, Ujenzi, Huduma za Bima, Mafuta na Gesi, Hoteli, Usalama, Bidhaa zinazotoka haraka, Matukio na Mapambo, Mitindo na Ubunifu, pamoja na Upigaji picha.

“Katika kipindi cha miaka 4 iliyopita, tumeweza kufikia maelfu ya wateja barani Afrika kupitia njia ya mtandao na kukusanya maoni yao juu ya bidhaa na huduma wanazotumia na zaidi ya tuzo 70 zimekuwa zikitolewa kila mwaka. Tunajivunia mafanikio haya”. alisema.

Akizungumzia mchakato wa kuwapata washindi, Diana alibainisha kuwa washindi wa tuzo hupatikana kupitia utaratibu wa kupiga kura mtandaoni ambapo walaji wana nafasi ya kupigia kura bidhaa au huduma mbalimbali zinazoshindanishwa kupitia tovuti ya CCAA”.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Latifa Khamis (wa tatu kushoto) akiwa ameshika mkasi tayari kwa ajili ya kuzindua rasmi tuzo za Consumer Choice Awards Africa(CCAA). Wapili kulia ni Diana Laizer ambaye ni mwanzilishi wa tuzo hizo na wengine katika picha ni wadhamini wa tuzo.

“Baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa washiriki katika makundi tofauti, timu yetu inafanyakazi ya kupanga makundi hayo kulingana na mapendekezo na vigezo vya tuzo husika. Zoezi hili likikamilika makundi huwekwa mtandaoni na walaji huweza kupiga kura kulingana na machaguo yao. Upigaji kura hufanyika kwa siku zisizopungua 25 na mlaji anaweza kupiga kura mara moja tu katika kila aina ya tuzo,” alifafanua.

Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi wa tuzo za Consumer Choice Awards Africa (CCAA) wakifuatilia matukio wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Diana, baada ya muda wa kupiga kura kumalizika, mfumo huonyesha matokeo kulingana na idadi ya kura ambazo bidhaa au huduma imepigiwa.

“Dirisha la kupendekeza aina za tuzo kwa mwaka 2023 limefunguliwa rasmi kuanzia leo tarehe 18 Juni 2023 na litaendelea hadi tarehe 9 Julai 2023. Zoezi  la upigaji kura litatangazwa baadaye mwaka huu kwahivyo tunayahimiza makampuni na chapa kushiriki na kushirikisha wateja wao,” aliongeza.

Mkurugenzi huyo aliyapongeza makampuni ambayo yamekuwa yakishiriki na kuwahamasisha wateja wao kuyapigia kura.

Leave a Comment