
Walinzi wa Ikulu ya Niamey nchini Niger, wamemuweka kizuizini rais wa nchi hiyo, Mohamed Bazoum huku wanajeshi wa nchi hiyo wakiizingira ikulu katika kile kinachotajwa kuwa ni jaribio la kumpindua rais huyo.
Vuguvugu hilo lililoanza asubuhi ya leo Jumatano, Julai 26, 2023 linatajwa kufanana na majaribio ya mapinduzi yaliyotokea katika nchi za jirani za Mali na Burkina Faso tangu 2020.
Majengo kadhaa ya serikali yakiwemo ya wizara mbalimbali nayo yamedhibitiwa na wanajeshi wenye silaha, wakiwazuia watu kuingia wala kutoka kwenye ofisi na nyumba za makazi zilizopo kwenye majengo hayo.
Wakati hayo yakiendelea, shughuli za kawaida kwa wananchi, zinaendelea kama kawaida.
Hii ni mara ya pili kwa Bazoum kukumbana na misukosuko ya kutaka kupinduliwa, ambapo Machi 2021, siku chache kabla ya rais huyo kuapishwa, kulitokea jaribio lingine la kumpindua.