
Dar es Salaam 29 Julai 2023: Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, leo amegawa vitendea kazi kwa Wajasiriamali 580 kwenye mradi wa Chipsika Kiajira na Coca Cola unaoendeshwa na Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola Kwanza ya jijini Dar es Salaam.
Akiwakabidhi vifaa hivyo, Zungu aliwaonya wafanyabiashara hao kuacha mambo ya anasa kama vile kuendekeza ngono, ulevi na mengineyo baada ya kuanza kuona faida.
Amewaasa kuwa mambo hayo ndiyo chanzo kikubwa cha kufilisika kuwa fukara kwa ujumla kwani biashara haiwezi kuendelea katika mazingira kama hayo.
Baadhi ya vifaa alivyowapa wajasiriamali hao ni pamoja na mitungi ya gesi ya kilo 15, majiko, mavazi ya kazi yaani ‘eplon’ na kofia, na vinginevyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Coca Cola Kwanza, Bwana Unguu Sulay amewapongeza Chuo cha Ustawi wa Jamii na Kampuni ya Gas ya Oryx kwa kuungana nao katika mpango wao wa kuwaendeleza wajasiriamali hao na kusema;
“Nianze na kuwapongeza sana Chuo cha Ustawi wa Jamii kwa kuwapa elimu Wajasiriamali hawa katika kampeni yetu hii ya Chipsika Kiajira ambao naamini itawasaidia katika biashara kuendeleza biashara zao na kuwatofautisha na mtu mwingine ambaye hajapata elimu kama waliyopewa wao na wataalam.
“Pia niwapongeze na Kampuni ya Oryx Gas kwa kuungana nasi na kukubali kuwapa hawa Wajasiriamali mitungi ya gesi na kuwafanya sasa wapike vyakula vyao kwa nishati safi na kuwaondolea hadha ya moshi walaji na wapishi jambo lililokuwa kero kwa wapika vyakula wengi haswa wauza chipsi na mama lishe”. Alisema Unguu.

Mkurugenzi huyo alimalizia kwa kusema kampeni ya Chipsika Kiajira lengo lake kuu si kujitangaza au kutaka kujizolea umaarufu bali ni uzalendo na kurejesha faida kwa jamii inayotumia bidhaa zao.
“Kama ni kutaka umaarufu tu basi tungeweza hata kudhamini mambo mbalimbali kama vile marathon na michezo mingine lakini tumeamua kurejesha tunachokipa kwa jamii ambayo imekuwa ikituunga mkono siku zote”. Alimaliza kusema Unguu.
Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya Oryx Gas, Ibrahim Fundi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Mauzo Kanda ya Mashariki aliyemwakilisha mkurugenzi wa kampuni hiyo ameupongeza mradi wa Chipsika Kiajira na kusema kusema utasaidia kuwakomboa Wajasiriamali wengi watakaoweza kutekeleza vyema waliyofundishwa.
Fundi amesema Oryx wako kwenye kumsapoti Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha kila mwananchi anatumia nishati safi ya kupikia.
“Matumizi ya Oryx Gas kama nishati safi ya kupikia itasaidia kutunza mazingira kwani hata vitendo vya ukataji miti hovyo kwa ajili ya mkaa na kuni yatapungua hivyo miti kuweza kustawi vizuri na kusababisha hata mvua zinyeshe kwa wakati”. Alimaliza kusema Fundi.