
Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump amelalamikia muda na gharama iliyotumika katika mapambano yake mengi ya kisheria na kuitaka Mahakama ya Juu zaidi kuingilia kati huku akidai kuwa mpinzani wake wa kisiasa amempiga kwa mfululizo wa mashitaka dhaifu ikiwa ni pamoja na DA, AG, na wengine, ambayo yanahitaji kiasi kikubwa cha muda na pesa kuzishughulikia.
Trump ameyasema hayo kupitia mtandao wa Truth Social ikiwa ni siku moja baada ya kufikishwa mahakamani kwa mara ya tatu ambapo alikana mashtaka manne ya jinai siku ya Alhamisi kuhusiana na uchunguzi wa wakili maalum Jack Smith kuhusu jaribio la kutengua uchaguzi wa urais wa 2020.
“Rasilimali ambazo zingeingia kwenye Matangazo na Mikutano, sasa itabidi zitumike kupigana na Majambazi hao wa mrengo wa kushoto katika mahakama nyingi nchini kote. Ninaongoza katika Kura zote, ikiwa ni pamoja na dhidi ya Crooked Joe, lakini huu si uwanja wa usawa. Ni Kuingilia Uchaguzi, na Mahakama ya Juu lazima iingilie.” Amesema Trump.
Akitoa maelezo mafupi baada ya kusikilizwa kwa kesi ya Alhamisi kabla ya kupanda ndege binafsi kurejea New Jersey, Trump alisema anachofanyiwa ni mateso kwa mpinzani wa kisiasa na kwamba haya hayakupaswa kutokea Marekani.
“Haya ni mateso ya mtu ambaye anaongoza kwa idadi kubwa sana katika mchujo wa Republican na anayemzidi Biden kwa kura. Kwa hiyo ukishindwa kumpiga unamtesa au unamfungulia mashitaka. Hatuwezi kuruhusu hili kutokea Marekani.” alisema Trump.