
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Bw. Alex Msama ametoa wito kwa mamlaka husika kuwachulia hatua wale wanaomkashifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia mitandao ya kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 12,2023 amesema kuwa Watanzania wanapaswa kumheshimu Mhe. Rais Dkt. Samia, kwani Mwenyezi Mungu ametupa mtu ambaye anaendelea kufanya kazi vizuri kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.
Amesema wale wote ambao hawana maadili kuacha mara moja kumkashifu Mhe. Rais kutokana na kwamba amekuwa anafanya kazi vizuri ili kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kuimarika, pia Mhe. Rais ni Mama wa familia kama walivyo wazazi wa kila mtu hivyo basi waache kutoa kauli ambazo sio rafiki zinazomdhihaki.
“Kwa siku za hivi karibuni kumeibuka kikundi cha watu wachache ambao kutokana na nia yao ovu dhidi ya Taifa la Tanzania na kwa maslahi yao binafsi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kubeza kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya Watanzania wote, binafsi Sifurahishwi na maneno ya kejeli yanayoelekezwa kwa kiongozi mkuu wa nchi, hivyo ninaomba mamlaka zinazohusika kuanza kuchukua hatua za kisheria kwa wanaotumia mitandao ya kijamii kumtusi Rais wetu, Dkt Samia Suluhu Hassan.”
“Pia natoa pongezi kwa kamati kuu ya chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutoa elimu ya uwekezaji kwa watanzania hivyo Watanzania wengi wameanza kuwa na uwelewa mkubwa kuhusu uwekezaji kwani baadhi walikuwa wanapotosha watu. Wapo baadhi ya watu wanataka kuchafua amani ya nchi yetu, vyombo vya usalama naomba wawachukulie hatua ili kuhakikisha amani ya nchi yetu inaendelea kuwa imara” amesema Bw. Msama.
Amefafanua kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia ameendelea kufanya kazi vizuri ikiwemo kuhakikisha wawekezaji wanaendelea kuwepo nchini.