
Mchezaji wa timu ya Taifa ya Panama Gilberto Hernandez, ameuawa kwa kupigwa risasi jana katika Mji wa Colon.
Watu walio na silaha walishambulia kundi la watu ambamo kati yao alikuwemo Mwanasoka huyo.
Hernandez (26), alifariki dunia na watu wengine saba walijeruhiwa.

Uchunguzi juu ya mauaji hayo bado unaendelea na bado haijajulikana kama watu hao walimlenga mchezaji huyo au la.
Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la mauaji katika Mji wa Colon kutokana na mivutano kati ya magenge mawili makubwa yanayogombania njia za usafirishaji wa dawa za kulevya.
Mwaka huu pekee zaidi ya watu 50 wameuawa katika mji huo wenye wakazi takribani 40,000.
Shirikisho la soka la Panama na klabu aliyokuwa akiichezea Hernandez wametuma salamu za rambirambi kwa familia.