
Winga wa Manchester United, Antony ameondolewa kwenye kikosi cha timu ya Taifa hilo kufuatia madai ya kumshambulia kimwili mpenzi wake wa zamani (EX)
Kupitia taarifa yake kwa umma, Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) limebainisha kufikia uamuzi huo baada ya aliyekuwa mpenzi wa nyota huyo, Gabriela Cavallin kumshutumu kwa kumpiga.

“Kutokana na ukweli uliojidhihirisha siku ya Jumatatu (Septemba 04) kuhusu mchezaji wa Man United Antony, ambao ni lazima uchunguzwe, na ili kumlinda mwathirika, mchezaji, timu ya taifa ya Brazil na CBF, shirikisho linauarifu umma kwamba mwanasoka huyo ameondolewa kwenye timu ya taifa ya Brazil.” imesema taarifa ya CBF
Cavallin alifichua kwamba amewasilisha malalamiko yake kwa Polisi wa Sao Paulo na Polisi wa Greater Manchester ambapo amesema Antony alimshambulia kwa nyakati tofauti kati ya Juni 2022 na Mei 2023.
Tukio moja lilihusisha kumrushia glasi, ambayo lilimchana hadi mfupa wa kidole chake ukaonekana.
Aidha katika shambulio lingine lililotokea alipokuwa mjamzito, Cavallin amefichua kuwa Antony (23), alimvamia wakiwa kwenye gari, na kutishia kumtupa kutoka kwenye gari lililokuwa likitembea na kuashiria kuwa angemuua yeye, mtoto na kujiua yeye mwenyewe.