
MAHAKAMA ya juu zaidi ya Australia imekataa ombi la Qantas la kubatilisha uamuzi kwamba ilifuta ajira 1,700 kinyume cha sheria wakati wa janga la corona
Mahakama ilikubali kwa kauli moja kwamba mtoa huduma huyo alikuwa amewafuta kazi kinyume cha sheria katika viwanja vya ndege 10 mnamo Novemba 2020.
Uamuzi huo uligundua kuwa Qantas ilikiuka Sheria ya Kazi ya Haki ya Australia, ambayo inalinda haki za wafanyikazi.
Qantas iliomba msamaha, lakini ikasisitiza kuwa ilikuwa hatua muhimu ya kifedha wakati wa Covid.
Shirika hilo la ndege liliwatimua washika mizigo na wasafishaji katika viwanja vya ndege kote Australia wakati taifa lilikuwa limefunga mipaka yake na biashara ilikuwa ikidorora.
“Kama tulivyosema tangu mwanzo, tunasikitika sana athari za binafsi za uamuzi kwa wale wote walioathiriwa na tunaomba radhi kwa dhati,” ilisema katika taarifa Jumatano.
Mahakama Kuu ya Australia ilikubali kwamba wakati Qantas ilikuwa na “sababu nzuri za kibiashara” za hatua hiyo, ilikuwa imewanyima wafanyakazi haki zao za “kushiriki katika hatua za kiviwanda zinazolindwa na…majadiliano.”
Wafanyakazi na wanachama wa vyama vya wafanyakazi walielezea matokeo kama “ushindi mkubwa” baada ya pambano la “Daudi na Goliathi”.
Chama cha Wafanyakazi wa Uchukuzi kilisema matokeo hayo ni uthibitisho kwamba “bodi nzima ya Qantas lazima ibadilishwe na wakurugenzi wapya akiwemo mwakilishi wa wafanyikazi”.
Qantas imekabiliwa na hasira ya umma katika wiki za hivi karibuni, baada ya kuvuna faida huku kukiwa na safu ya kashfa zinazohusiana na vitendo vyake wakati wote wa janga la corona. Shirika hilo la ndege pia lilishutumiwa kwa kuunga mkono kizuizi cha serikali katika upanuzi wa safari za ndege za Qatar Airways kwenda na kutoka Australia, hatua ambayo wakosoaji wanasema ingelifanya soko liwe na ushindani zaidi na kupunguza nauli.