×

Naibu Waziri wa Uchukuzi: Mchakato wa Kutafuta Mfumo Bora wa Namna ya Kupeleka Mifugo nje Umeanza

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amesema Wizara ya Uchukuzi imeanza mchakato wa kutafuta mfumo bora wa namna ya kupeleka mifugo nje ikiwa imechakatwa kama nyama au mifugo kama ilivyo.
Naibu Waziri amesema hilo litafanikiwa kwa sababu ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yeye anatembea kwenye sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ndio maana amepandisha kiwango cha bajeti alichokikuta kwenye mifugo na kilimo.
“Nchi yetu ni ya Pili kwa Mifugo Barani Afrika, Lakini Majirani zetu ndio wanapeleka ng’ombe wengi zaidi nje ya bara letu, Uongozi uliopo sasa chini ya Mhe Rais Samia umefanya mapinduzi Makubwa kwenye Sekta hizi za uzalishaji. Mfano Mifugo peke yake Mhe. Rais alikuta bajeti ya bilioni 66 sasa iko bilioni 294, kwenye kilimo amekuta bajeti bilioni 294 leo ni bilioni 960.
Taifa la Tanzania limebarikiwa ng’ombe Milioni 36.5, mbuzi milioni 25.6, kuku, pamoja na mabata milioni 90 lazima tuanze kuangalia miundombinu ya uchukuzi wa kupeleka mifugo hiyo na chakula nje ya nchi ukoje ili kuunga mkono jitihada nzuri sana za Waizara za Kilimo na Mifugo.
Tayari kama wizara tumeanza kuchakata mfumo bora wa namna ya kupeleka mifugo yetu nje iwe imechakatwa kama nyama au mifugo kama ilivyo”
Pia ametoa fursa kwa wamiliki wa maboti kupeleka boti zao Pangani kwa ajili ya usafiri na kuahidi kama kutatakiwa maboresho Wizara itafanya hivyo.
“Pale kwako Mheshimiwa DC (Pangani) tumetengeneza Gati tunatoa wito kwa wasafirishaji wapeleke maboti yao pale na tupo tayari kuendelea kuboresha zaidi kama itaonekana kuna huo uhitaji.
Bidhaa kubwa wanazotumia watu pale ni mafuta ya kula, chakula, vifaa vya ujenzi, zikiwemo na mbao.
Wizara chini ya Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa iko tayari kushirikiana na Pangani na wadau wote kusukuma Sekta hizi muhimu.”

Leave a Comment