
KOCHA Mkuu wa Yanga, Muargentina, Miguel Gamondi, anafahamu wapinzani wao Azam FC wataingia kwa kupania, lakini hiyo haofii yeye kupata ushindi katika mchezo huo.
Timu hizo zinatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, Jumapili hii katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Mchezo wa mwisho ambao ulizikutanisha timu hizo, katika Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Clement Mzize na Kennedy Musonda.
Akizungumza na Spoti Xtra, Gamondi alisema anaiheshimu Azam kutokana na ubora wa wachezaji ambao imewasajili huku akiamini mchezo huo utakuwa mgumu.

Gamondi alisema ugumu wa mchezo huo utaongezeka kutokana na kipigo hicho ambacho waliwapa Uwanja wa Mkwakwani, hivyo hawatakubali wachezaji na viongozi wataingia uwanjani kwa kupania kulipa kisasi, atacheza kwa tahadhari kubwa ya kujilinda na kushambulia ili wapate pointi tatu.
Aliongeza kuwa anataka kuona wachezaji wake wakicheza kwa kiwango kikubwa ndani ya dakika zote 90, tofauti na mchezo uliopita wa Ngao ya Jamii ambao vijana wake walicheza vizuri zaidi kipindi cha pili.
“Kama kocha tayari nimefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo, kwa kuwapa mbinu tofauti za ushindi kuelekea mchezo huo ambao muhimu kwetu kupata ushindi ili tukae kileleni.
“Ninafahamu Azam wataingia uwanjani kwa kucheza kwa kutupania, ni kitu ambacho ni kawaida kwetu Yanga kwani kila timu inayokutana na sisi inabadilika na kutupania, hivyo hilo alinipi hofu.
“Wachezaji wangu wote waliokuwepo katika majukumu yao ya timu za taifa, wameripoti kambini isipokuwa Aucho (Khalid) na Diarra (Djigui) wenyewe wanatarajiwa kuripoti kambini leo (jana Jumatano) baada ya kumaliza michezo yao ya kitafiki.
STORI NA WILBERT MOLANDI