
SERIKALI inaendelea kuhakikisha sekta ya anga inafanyiwa maboresho makubwa kwa ununuzi wa ndege, kuboresha viwanja vya ndege na ununuzi wa rada nne za kuongozea ndege, Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imeendelea kuhakikisha kwamba malengo hayo ya serikali yanatokea nchini.
Hayo yamemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Abdallah Komba katika mbio za kujifurahisha ziliyoandaliwa na TCAA za Km tano hadi Km 10 ikiwa ni katika muendelezo wa kuadhimisha miaka 20 ya mamlaka hiyo.

“Rais anaipa kipaumbele eneo la anga ili kuruhusu Tanzania iweze kufikika kupitia anga, kazi kubwa inafanyika katika kuboresha viwanja vya ndege na tayari TCAA inaendelea kutoa huduma kwenye viwanja 15 katika Taifa letu,” amesema Komba.
Pia, amesema shirika hilo la ndege limeendelea kuimarisha, ambapo hadi sasa tunazo ndege takribani 13 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa sekta ya anga Tanzania.
Komba amesema uboreshwaji wa sekta ya anga, reli na miundombinu katika sekta ya maji unalenga kuifanya Tanzania ifikike kwa mazingira tofauti tofauti nchini.
“Mamlaka ya usafiri wa anga nyie ndiyo askari namba moja mnaotegemewa na Rais kuifanya Tanzania ifikike kwenye Kona zote za Dunia,”

“Kutokana na umadhubuti na umakini walionao TCAA pamoja na ufanisi wao, viwanja vya ndege nchini vitaendelea kuwa imara wakati wote na anga litaendelea kuwa salama ambapo itapelekea kupokea makampuni mengi ya ndege kutoka duniani kuja Tanzania.” Aliongeza
Komba aliwapongeza TCAA kwa kuhakikisha kunakua na chuo cha mafunzo ya muda mfupi ya wataalamu wa sekta hiyo na kuwataka kuendelea kuimarisha chuo hicho lakini pia kuhakikisha kunakuwepo na wataalamu wa kutosha ili kuendelea kuzalisha wataalamu wengi zaidi ambao wataendelea kusaidia katika ukuaji wa sekta hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alitoa wito kwa
wana anga wote, watumishi na watanzania kwa ujumla kujali afya zao , kuzingatia mlo na kufanya mazoezi kwani mazoezi ni tiba na ni sehemu ya afya ambayo itasaidia kuepuka magonjwa nyemelezi na kuhatarisha maisha.
Mbali na hayo amesema kesho wanatimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake ambapo watakua na mkutano mkubwa wa Wana anga huku mgeni rasmi akiwa ni waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ambapo watazungumzia waliotoka tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo na wanapokwenda kwa miaka ijayo.
Naye Lugalo Masomola kutoka LATRA ambaye katika mbio hizo alikimbia km 5 amesema mashindano yalikua mazuri na atajitahidi kufanya vizuri zaidi kwa mashindano yajayo.