×

Netanyahu apinga Palestina kuongozwa na chama cha Mahmoud Abbas baada ya vita vya Gaza

Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari jana usiku, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema jambo ambalo litakuwa limezua taharuki mjini Washington.

Alipoulizwa kuhusu utawala wa baadaye wa Ukanda wa Gaza, alisema anapinga kurejeshwa kwa Mamlaka ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa Magharibi (PA), inayoongozwa na Rais mzee wa Palestina Mahmoud Abbas.

“Itabidi kuwe na kitu kingine,” alisema.

“Hakuwezi kuwa na mamlaka ambayo haikulaani mauaji hayo [tarehe 7 Oktoba na Hamas].”

Pia alirudia msisitizo wake kwamba Israel itadumisha udhibiti wa usalama Gaza. “Sitahatarisha udhibiti wa usalama kwa hali yoyote.”

Wakati wa safari yake ya hivi majuzi katika eneo hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alimwambia Bw Abbas kwamba Washington iinakiona chama chake cha PA kama chama “kitakachochukua jukumu kuu” huko Gaza baada ya kushindwa kwa Hamas.

Netanyahu ameweka wazi ni nani hataki aitawale Gaza katika siku zijazo: Hamas au PA. Lakini hadi sasa hajatoa njia mbadala.

Pamoja na kuongezeka kwa wasiwasi wa kimataifa juu ya gharama ya maisha ya Wapalestina ya operesheni ya kijeshi ya Israeli huko Gaza, kukataa kwa Netanyahu jukumu la PA kunamuweka katika hali ya msuguano na mshirika mkuu wa Israeli, Marekani.

Leave a Comment