×

Serikali Kusimamia Watanzania Wengi Zaidi Kushiriki Fursa Za Kiuchumi Migodini

Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde

Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia S. Hassan umedhamiria kusimamia sheria ili kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanashiriki kwenye uchumi wa madini kupitia usambazaji wa bidhaa na kutoa huduma kupitia migodi nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde jijini Dar es salaam Novemba 25, 2023 wakati wa mahafali ya Chuo cha Mitambo na Teknolojia(IHET) yaliyofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza.

“Serikali kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilifanya marekebisho ya sheria kwa lengo la kusimamia ushiriki wa watanzania kwenye uchumi wa madini ili fursa nyingi zitokanazo na uwekezaji kwenye sekta ya madini ziweze kuwanufaisha watanzania kupitia Ajira,utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa.

Wizara ya Madini itahakikisha inasimamia kwa dhati utekelezaji wa matakwa ya sheria hii ili kuongeza wigo wa watanzania katika ushiriki wao kwenye sekta ya madini.

Ninawapongeza sana Chuo cha IHET kwa kuzalisha wataalamu ambao ni waendesha mitambo mikubwa ambayo kwa kiasi kikubwa ndio inayotumika migodini.

Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kikiwemo chuo cha IHET ili kuhakikisha tunawaandaa watanzania wengi zaidi kukidhi vigezo na ubora katika usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini”Alisema Mavunde

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha IHET Prof. Patrick Makungu amesema mahafali haya ya tatu yanakamilisha zaidi ya wahitimu 2000 ambao chuo kimewazalisha tangu uanzishwaji wake na kwamba dhamira kuu ya chuo cha IHET ni kuzalisha wataalamu wenye weledi,ubora,maadili na shindani katika soko la Ajira ili pia kuongeza nafasi ya watanzania kushiriki katika sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo masuala ya nishati,madini,uchukuzi na ujenzi.

Leave a Comment