
KIUNGO mshambuliaji fundi wa Yanga raia wa Ivory Coast, Pacome Zouzoua, ameahidi kuipambania timu yake watakapocheza dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Kauli hiyo imekuja baada ya Yanga mchezo wa kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kufungwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya nchini Algeria.
Yanga iliyopo Kundi D, Jumamosi ya wiki hii inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kumenyana na Al Ahly.
Akizungumza na Spoti Xtra, Pacome alisema wachezaji na benchi la ufundi wote wamesahau matokeo yaliyopita dhidi ya CR Belouizdad na badala yake akili na nguvu zao wamezihamishia kwa Al Ahly.
Pacome alisema katika mchezo huo, wanakwenda kushinda na siyo kitu kingine ili kuhakikisha wanajiwekea mazingira ya ushindi hasa mechi za nyumbani, huku akibainisha kwamba, yeye binafsi atahakikisha anatengeneza nafasi za kufunga pamoja na kufunga mwenyewe.
“Kwanza nianze kwa kushukuru kurejea salama nyumbani, na moja kwa moja kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Al Ahly.
“Pili, tunajiandaa kufanya vizuri kuhakikisha tunashinda mechi hii, binafsi nitafanya juhudi kuona nafunga au kutengeneza nafasi ya kufunga,” alisema Pacome.