×

SBL Yaungana na Kampuni Tanzu ya Umoja wa Mataifa Kwenye Malengo Endelevu

 

Kampuni ya bia ya Serengeti Breweries Limited leo imetia saini makubaliano ya kuwa mwanachama wa UN Global Compact (UNGCT) na kujiunga rasmi kwenye idadi ya makampuni makubwa duniani yanayoshirikiana na Umoja wa Mataifa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kupitia programu mbalimbali endelevu.

SBL ambayo inajulikana kwa programu zake za kijamii nchini Tanzania kama vile kwenye maeneo ya utunzaji wa vyanzo vya maji safi na salama; unywaji pombe kistaarabu; ujumuisishwaji na ushirikishaji; upandaji miti na miongoni mwa mambo mengine, kampuni hio pia imejitolea kuendelea kusaidia matokeo chanya kwa jamii hadi ifikapo 2030 kulingana na tarehe ya mwisho iliyowekwa na Umoja wa Mataifa kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

Akizungumza katika utiaji saini ya makubaliano ya ushirikiano kwenye hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurgenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi alinukuliwa, “Uendelevu ni jambo la msingi sana kwenye biashara yetu kuhakikisha tunachangia kwenye maendeleo chanya ya jamii inayotuzunguka ambayo kwayo tunavuna malighafi yetu, kuishi, pamoja na kuuza bidhaa tunazozitengeneza’.

Marsha Mactta-Yambi, Mkurugenzi wa UNGCT pia aliipongeza kampuni ya SBL kwa hatua thabiti waliyoichukua kuimarisha jitihada za pamoja kwenye maendeleo. Alisema, ‘ushirikiano huu utaenda kufungua fursa mpya na kudumisha nguvu za pamoja tulizoweka kuelekea 2030, tunaishukuru sana SBL kwa kuwa mwananchama mpya katika kufanikisha malengo tuliyoyaweka kwa pamoja.’

Kupitia mkakati wake wa miaka 10 ya kujenga jamii imara na endelevu iitwayo, ‘Society 2030 Spirit of Progress’, kampuni hio ya bia imechukua jitihada za awali kusaidia jamii ya kitanzania katika masuala kama upatikanaji wa maji safi na salama kwa kuchimba visima ishirini na tano (25) vilivyonufaishi takribani watu milioni mbili (2) nchini kote.

Halikadhalika, kampuni ya SBL inaendeleza miradi mbalimbali ya kuhifadhi maji kwenye viwanda vya mkoani Kilimanjaro, Mwanza na Dar es Salaam ili kupunguza matumizi ya maji kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2030.

Na ili kuendeleza upatikanaji wa nafaka kutoka kwa wakulima wa ndani, kampuni hio inaendesha mpango wa kilimo biashara na mtandao wa wakulima zaidi ya 400, ambao unahusisha kuwapa mafunzo juu ya mbinu za kilimo cha kisasa, Obinna alisema.

Vile vile kampuni hiyo miaka mitatu iliyopita ilizindua mpango wa ufadhili wa masomo uitwao, Kilimo Viwanda kwa wanafunzi mahiri kutoka jamii za wakulima ili kusaidia mpango wa kilimo biashara ambapo zaidi ya wanafunzi 230 wametunukiwa ufadhili wa masomo.

Leave a Comment