×

Knauf Gypsum Yatoa Msaada wa Vifaa vya Ujenzi kwa Wakazi wa Hanang

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri na Ilse Boshoff Mkurugenzi wa kampuni ya Knauf Kanda Afrika Mashariki wakipeana mikono kama ishara ya kupokea msaada wa vifaa vya ujenzi kutoka Kampuni ya Knauf unaokwenda kwa wahanga wa mafuriko ya maporomoko ya mlima wa Hanang, Mkoani Manyara. Msaada huo umetolewa katika Ofisi za TIC Dar es Salaam.

Kampuni ya uzalishaji wa vifaa vya ujenzi ya Knauf Gypsum Tanzania imeungana na Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi kwa wakazi wa Hanang walioathiriwa na mafuriko na maporomoko ya mlima yaliyosababisha vifo vya watu 89.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na gypsum boards, skimming plasters ambavyo vitatumika kusaidia ujenzi wa majengo yaliyoharibika.

Akiongea wakati wa kukabidhiwa msaada huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Gilead Teri alisema hatua ya kuwasaidia wakazi wa Hanang walioathiriwa na maafa iliyochukuliwa na Knauf Gypsum Tanzania ni ya kupongezwa na kuwataka wawekezaji wengine kuiga mfano.

“Kampuni ya Knauf imekuwa ndiyo ya kwanza kutufikia na kutueleza nia yao ya kutaka kuwasaidia wakazi wa Hanang. Baada ya kutufikia na sisi tuliwasiliana na ofisi ya Waziri inayohusika na mazingira ili kuweza kufikisha msaada kwa waathirika wa mafuriko na maporomoko,” alisema.

Ilse Boshoff Mkurugenzi wa kampuni ya Knauf Kanda Afrika Mashariki akiongea na waandishi wa Habari juu ya msaada wa vifaa vya ujenzi uliotolewa na kampuni ya Knauf kwa TIC kwenda kwa wahanga wa mafuriko ya Matope wa Hanang, Mkoani Manyara. Msaada huo umetolewa katika Ofisi za TIC Dar es Salaam.

Aliongeza “Huu ni mfano mzuri na bora kabisa kwa makampuni mengine kuiga kwa kuwa unaonyesha namna wanavyojali na kushirikiana na jamii hata wakati wa majanga na shida. Hii inakwenda sambamba na ule msemo wa Rafiki anayekujali wakati wa shinda ndiyo Rafiki wa kweli. Leo Knauf imetuonyesha kuwa ni Rafiki wa kweli,”

Kwa upande wake mkurugenzi wa Knauf Gypsum Tanzania Ilse Boshoff alielezea kampuni hiyo kuguswa na tukio la Hanang na kuona umuhimu wa kutoa msaada kwa jamii na wakazi wa eneo hilo na kuongeza kuwa kampuni hiyo ipo tayari kushirikiana na Watanzania katika hali zote.

“Tunajisikia furaha kufanya kazi na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya Watanzania. Kwa namna ya pekee, leo tunayo furaha kutoa msaada huu kwa wakazi wa Hanang utakaosaidia ujenzi wa majengo yaliyoharibiwa,” alisema

Leave a Comment