
Kampuni za Denmark zimealikwa kuja kuwekeza nchini katika sekta za uchukuzi, nishati, madini, mazingira na uchumi wa buluu ambazo ni moja ya sekta za kipaumbele za Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwaliko huo umetolewa wakati wa mikutano baina ya Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Masuala ya Hali ya Hewa wa Denmark, Dan Jorgensen na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo iliyofanyika jijini Dodoma Aprili 5, 2024.

Waziri Nchemba alisema Serikali inajenga miundombinu ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) ambapo Serikali ya Denmark imesaidia kipande cha kutoka Morogoro hadi Makutupora ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 90. Alisema Serikali inakaribisha wawekezaji kuendesha reli hiyo ambapo itakapokamilika itaunganisha Tanzania na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda.
Dkt. Nchemba pia alizitaka kampuni za Denmark kuchangamkia fursa za ujenzi wa barabara ya mwendo kasi (express way) ya kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo kuu nchini.

Kwa upande wake, Dkt. Jafo alisisitiza umuhimu wa Denmark kushirikiana na Tanzania katika programu za utunzaji wa mazingira ikiwemo uwekezaji katika sekta ya nishati jadidifu. Aliiomba Denmark kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Misaada inayohitajika, alisema kuwa ni pamoja na kujenga uwezo wa watumishi, misaada ya kiufundi na rasilimali mbalimbali zikiwemo fedha.
Prof. Mkumbo, kwa upande wake alisisitiza umuhimu wa kampuni za Denmark kuja kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani (processing industries) hususan katika madini hadimu nchini. Alisema fursa katika sekta hiyo ni kubwa kwa kuwa Tanzania ina takribani aina 10 za madini hayo.
Aliiomba Denmark kuunga mkono jitihada za Serikali za kuchochea ukuaji sekta binafsi nchini.