×

Serikali Ya Uingereza Yatangaza Mikakati Mipya Ya Ushirikiano Na Tanzania Katika Kuboresha Uwekezaji

Serikali ya Uingereza imetangaza mipango na mikakati mipya ya ushirikiano na Serikali ya Tanzania ili kuzimarisha ushirikiano katika Sekta za Afya, Uwekezaji na Biashara na kusaidia miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Mipango hiyo imetangazwa  Aprili 5, 2024 jijini Dodoma na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika,  Andrew Mitchell wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi Ndogo za Ubalozi wa Uingereza jijini hapa.

Akitangaza mipango hiyo, Mhe. Mitchell amesema Serikali ya Uingereza imechangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 18.9 kwenye Mpango wa Miaka Mitano wa Afya kwa Wote unaotekelezwa nchini ili kuimarisha mifumo ya afya, kuimarisha ustahimilivu wa huduma za afya, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Kadhalika, Uingereza imetoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 15 kwa ajili ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwenye masuala ya maboresho ya Afya ya Uzazi ikiwemo kuboresha huduma za uzazi wa mpango kwa lengo la kuwafikia takribani watu 900,000.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba

Katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususan kwenye kuboresha hali ya maisha ya Watanzania, Serikali hiyo imeahidi kuendelea kusaidia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) ambao hutoa ruzuku kwa asilimia 15 kwa kaya maskini zaidi katika mikoa yote ya Tanzania ili kuimarisha uchumi, upatikanaji wa chakula na kuboresha mazingira kwa kaya hizo.

Kadhalika Serikali hiyo imepongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo nchi hiyo katika kuunga mkono jitihada hizo imeahidi kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 6.9 hadi mwaka 2026 ili kuwezesha upatikanaji wa nishati safi na kukuza teknolojia safi ya kupikia kwa utunzaji mazingira.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kwa kutangaza mipango na ufadhili kwa miradi.

Leave a Comment