
Dar-es-Salaam, 11 Mei 2024: Ikiwa ni mwaka mmoja tangu kufariki kwa aliyekuwa mwanasiasa mkongwe hapa nchini, Hayati Benard Membe, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema imekuwa ni siku nzuri ya kutafakari kazi nyingi alizozifanya nchini hasa katika Jimbo ambalo alilokuwa akiliongoza la Mtama mkoani Lindi.
Akizungumza kwenye hayo leo kwenye ibada ya kumuombea marehemu huyo iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Jijini, Waziri Nape amesema kuwa yale mema aliyoyafanya wakati wa uhai wake na kuona namna gani ya kuendelea kuyaenzi na kutekeleza yale aliyokuwa akiyapigania kwa masrahi ya Watanzania.

“Tumeandaa misa hii kwa ajili ya kumkumbuka kaka yetu Benard Membe ambapo kesho tarehe 12 atakuwa anatimiza mwaka mmoja tangu afariki, tumekuwa na siku nzuri ya kutafakari kazi nyingi alizozifanya katika nchi yetu na Jimbo la Mtama alilowahi kuliongoza na ndipo pia alipozaliwa.”
“Kuna mambo aliyaanzisha na hapa ndiyo ilikuwa tafakari kubwa, kuna mambo aliyaanzisha kwa kanisa ambalo alikuwa akihudumiwa ikiwemo baadhi ya ujenzi wa makanisa na majengo mbalimbali ya kanisa, ambapo tumekubaliana tuangalie namna ambayo tutazikamilisha Zile ndoto alizozianzisha”amesema Waziri Nape.

Nae Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama amewataka Watanzania kuendelea kuyakumbuka na kuyaenzi mambo mema aliyoyafanya Hayati Benard Membe wakati wa uhai wake na kuona namna gani ya kuendeleza na kuyasimamia ili yatekelezwe.
Amesema Hayati Membe ameacha alama ndani ya serikali wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Kimataifa, kwani matunda na alama aliyoicha inaigusa nchi.

“Sasa unatimia mwaka mmoja tangu atutoke ambapo ametuachia mambo mengi, kuna mambo mengi amefanya katika taifa letu na kuna mambo mengine ambayo ametuachia ili sisi tuyaendeleze. Kikubwa ambacho ametuachia sisi watu wake wa karibu, tuwe wamoja, tuwe tunasameheana tunapokoseana, tusiwe watu wa visasi, tusiwe watu wa kuzungumziana mambo ambayo si sahihi na ametuachia tuwe wazalendo katika taifa letu ili tuweze kuwasaidia na wengine ambao wanatakiwa kuinuliwa”
“Tusisahau kumcha Mungu, tuwe tunajitolea sana katika kazi zake na kusaidia kwenye miradi ya mbalimbali ili kuufikia ufalme wa mbinguni na kuhakikisha kazi zake zinasonga mbele. Sisi kama watu tuliokuwa karibu na Hayati Membe, tunaendelea kuyaenzi yale aliyokuwa akiyapambania kwa masrahi ya Watanzania”alimaliza kusema Msama. HABARI/PICHA NA NEEMA ADRIAN /GPL