
Watu 11 wakiwemo raia watatu wa kigeni wamefariki dunia na wawili kujeruhiwa baada ya mtambo wa kuzalisha mvuke katika kiwanda cha sukari cha Mtibwa mkoani Morogoro kupata hitilafu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama amesema tukio hilo limetokea majira ya saa saba na nusu usiku wa kuamkia Mei 23, 2024.
Kamanda Mkama amesema raia wa kigeni waliofariki ni kutoka Kenya, India na Brazil.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali ya Mtibwa Sugar na majeruhi wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Misheni ya Bwagala.
Waliokufa ni wataalamu wa umeme na mitambo ambao walikuwa kwenye chumba cha kuendesha mitambo hiyo.
