
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini zihakikishe zinakamilisha uanzishwaji wa Madawati ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ifikapo Julai 2025.
Sambamba na hilo amesema, Halmashauri hizo pia zihakikishe masuala ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yanakuwa sehemu ya mipango na bajeti za kila mwaka, ili iwahudumie vijana wanaojishughulisha na masuala ya ubunifu, kufanya haya kutasaidia kuimarisha uwezo wa nchi katika tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu”

Ametoa maagizo hayo Ijumaa, Mei 31, 2024 katika Maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2024, yanayofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal jijini Tanga. Maadhimisho hayo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuongeza hamasa ya kukuza elimu, ujuzi na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI zihakikishe kuwa ifikapo Julai 2025 Shule zote za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi viwe vimeanzisha Majukwaa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu wa Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza bunifu 283 zilizotokana na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU). “Tayari bunifu 42 kati ya hizo zimeshaingia Sokoni na imewezesha kuanzishwa kwa kampuni 94 kutokana na bunifu na teknolojia zinazobuniwa na wabunifu wa Kitanzania.”
“Nitoe wito kwa wabunifu nchini, mmebuni kazi na kazi hizo zinamatokeo, jipangni kuboresha kazi zenu, fungueni kampuni na mtangaze biadhaa hizo.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeanzisha Vituo vya Umahiri 12 katika Taasisi za Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti na Maendeleo nchini. “Vituo hivyo vimeanzishwa kwa lengo la kuchagiza utafiti, ubunifu na ubiasharishaji wa matokeo yanayotokana na shughuli hizo”
