
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemteua Dkt. Ashura Abdul Katunzi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Kabla ya uteuzi, Dkt. Katunzi alikuwa Afisa Udhibiti Ubora Mkuu, Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Dkt. Katunzi anachukua nafasi ya Dkt. Athuman Yusuf Ngenya ambaye amemaliza muda wake.
Aidha, taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka imeeleza kuwa Dkt. Samia amemteua Bw. Hassan Juma Mnyika kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo. Kabla ya uteuzi, Bw. Mnyika alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu. Bw. Mnyika anachukua nafasi ya Bw. Lain Ephraim Kamendu ambaye amestaafu.
Vilevile Rais Samia amemteua Bw. Addo Missama kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi. Kabla ya uteuzi, Bw. Missama alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais Ikulu. Bw. Missama anachukua nafasi ya Bw. Joseph Constantine Mafuru ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
