
KATIBU wa Itikadi na uenezi na mafunzo wa Halmashauri kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amosi Makalla amesema suala la kuongezewa mhula wa Urais wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi halijazungumzwa na vikao vya chama, hivyo lililosemwa ni wazo tu la mtu.
Akizungumza na Global Tv leo, Makalla amesema wazo hilo amelisikia na kusoma kwenye magazeti ya leo Junie 24, 2024 lakini kwenye vikao halali vya chama hakusikia kitu kama hicho.

“Mimi naingia kwenye vikao vyote vya juu vya chama kuanzia cha sekretarieti, Halmashauri kuu ya Taifa, Kamati kuu na mkutano mkuu wa CCM lakini hilo jambo halijawahi kuzungumzwa.
“ Niwatoe hofu Watanzania wote kwa kuwaambia kwamba hilo ni wazo tu la mtu. Mimi huwa nazungumzia mambo ya chama yaliyojadiliwa na vikao, mimi ndiye msemaji, hilo (la kuongezewa muda wa urais wa Zanzibar) halipo,” alisema Makalla.
Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa, Katibu huyo wa uenezi alisema yeye hana wasiwasi nao kwa sababu CCM imejipanga tangu ngazi ya chini.

“CCM imejipanga na ina mizizi tangu kwenye wajumbe wa nyumba kumi kumi, kwenye matawi, kata, wilayani hadi mkoani, tofauti na wenzetu ambao wao wanazungumzia majimbo ambapo kiongozi anakuwa na mikoa zaidi ya mitatu, hivyo wapinzani hawawezi kutushinda.
“Kuhusu ushindi sisi CCM tunaangalia asilimia kwamba tuwe na asilimia kubwa na sio kushindwa na ndio maana utaona tunashinda chaguzi nyingi,” alifafanua Makalla.
Akizungumzia suala la Tume Huru ya Uchaguzi alisema wapinzani siku zote wao huisifia tume hiyo wakishinda lakini wanaposhindwa hulalamika kwamba inapendelea. Alisema hilo wanalijua na anajua kwa nini wanafanya hivyo.

