
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, ametangaza kuwa anasimama na raia wa Kenya na kuitaka serikali ya rais Ruto kuwasikiliza wananchi badala ya kutumia nguvu zinazoweza kuliweka taifa kwenye njia panda na vurugu zaidi.
“Ninakuja kwenu nikiwa na huzuni kubwa ya kupoteza maisha kutokana na hali ya sasa nchini. Ni haki ya Wakenya kuandamana kama ilivyoamuliwa na Katiba ya Kenya ya 2010. Pia ni wajibu wa viongozi kuwasikiliza wanaowaongoza,” Kenyatta amesema.
“Kama rais wenu wa zamani nimehisi uzito wa kuwaongoza Wakenya. Kwa hivyo naomba hekima na ustaarabu uimarishwe na amani na maendeleo yawe yetu sote kama watoto wa Kenya,” ameongeza.
Wakenya wanaofanya maandamano makubwa katika miji mikuu wanaendelea kuongeza shinikizo kwa serikali ya Rais Ruto kuuondoa kabisa Mswaada wa Fedha wa 2024 uliobeba makato ya ushuru kufadhili bajeti ya 2024/25 na ambayo yameibua joto jingi.
Bunge la taifa Jumanne, limepitisha mswaada huo, wabunge 195 walipiga kura ya NDIO huku wabunge 100 wakipiga kura ya LA, na rais Ruto anatarajiwa kuufanya kuwa sheria wakati wowote.
