
Mwanamke mmoja amekuwa mtu wa kwanza kufungwa jela chini ya sheria inayopinga ndoa ya lazima nchini Australia, kwa kummlazimisha binti yake mwenye umri wa miaka 21 kuolewa na mwanamume ambaye baadaye alimuua.
Sakina Muhammad Jan, ambaye ana umri wa karibu miaka 40, alipatikana na hatia ya kumlazimisha Ruqia Haidari kuolewa na Mohammad Ali Halimi mwenye umri wa miaka 26 mwaka wa 2019, kwa malipo kidogo.
Wiki sita baada ya harusi, Halimi alimuua mke wake mpya – alipatikana na hatia na sasa anatumikia kifungo cha maisha jela.
Siku ya Jumatatu, BiJan – ambaye alikana hatia – alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela, kwa kile hakimu alichokiita “shinikizo lisilovumilika” aliloweka kwa binti yake.
Sheria za kupinga ndoa za kulazimishwa zilibuniwa nchini Australia mwaka wa 2013 na adhabu ya juu zaidi ya kifungo cha miaka saba.
Kuna kesi kadhaa zinazosubiri kuamuliwa, lakini Jan ndiye mtu wa kwanza kuhukumiwa kwa kosa hilo.