
MBUNGE wa Buchosa, mkoani Mwanza, Mhe. Eric Shigongo James ameishukuru Serikali kwa kuonesha juhudi kubwa za mapambano dhidi ya janga la Mamba kula wananchi katika maeneo ya Ziwa Victoria, jimboni Buchosa.
Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mhe. Shigongo alisema tangu awasilishe hoja binafsi Bungeni jijini Dododoma miezi mitatu iliyopita kuitaka Serikali ikomeshe janga la Mamba Buchosa, tayari vizimba vinne vimeshajengwa katika maeneo tofauti tofauti, ikiwa ni jitihada za kupambana na janga hilo.
Alisema, vizimba hivyo vimejengwa katika maeneo ya Chitare, Nyakalilo, Izindabo na Kanyala.

“Ninaishukuru sana Serikali kwa kutujengea vizimba hii vinne, lakini ukweli ni kwamba bado janga la Mamba kula wananchi linaendelea kwa kasi sana Buchosa, juzi tu tarehe 20 mwaka huu, mama mmoja ameliwa na Mamba wakati akiosha vyombo, hakika inauma na kusikitisha sana kuona wananchi wanaangamia kwa kuliwa na Mamba.
“Dawa ya kupunguza na kukomesha janga la Mamba Buchosa ni kujenga visima kandokando ya Ziwa Victoria ili wananchi wasichote maji wala kuogea ziwani, tunaomba anagalau tujengewe visima 15, ambavyo nina uhakika vitapunguza kwa kiasi kikubwa Sakata hili la Mamba kula wananchi,” alisema Mhe. Shigongo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Shigongo aliishukuru Serikali ya awamu ya sita, kwa kupelekea miradi mingi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 60 katika huduma mbalimbali za kijamiii ikiwemo elimu, afya, maji, nishati ya umeme na miundombinu ya barabara.