
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inatarajiwa kuanza safari za ndege ya mizigo nchini Komoro baada ya kuongezeka kwa uhitaji baina ya wafanyabiashara wa nchi zote mbili.
Safari hizo zitaanza rasmi Septemba 13 mwaka 2024 kwa kutumia ndege ya mizigo aina ya Boeing B767-300F yenye uwezo wa kubebea tani 54 za mzigo kwa mara moja na kuruka kwa wastani wa masaa saba hadi 10 bila kutua.
Mkuu wa Kituo cha ATCL upande wa Komoro, Esther Maiga ameyasema hayo wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Komoro, Mhe. Said Yakubu ubalozini, Agosti 29, 2024 alipokuwa akimtambulisha mwakilishi wa ComAir ambaye ni Wakala wa ATCL nchini Komoro, Kamarouddine Waziri Zamane.

“Hivi sasa ATCL tunafanya safari tatu kwa wiki baina ya Dar es Salaam na Moroni na tunatarajia kuongeza safari hadi kufikia nne kwa wiki. Safari ya nne itakuwa ni ndege ya mizigo B767-309F ambayo tunatarajia kuanza miruko tarehe 13 Septemba, 2024”, amesema Esther na kuongeza;
“Kuongezwa kwa safari hii ni muitikio kwa jumuiya ya wafanyabishara wa Tanzania na Moroni ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiomba huduma ya kusafirisha bidhaa zinazoharibika haraka kutokana na jiografia ya nchi ya Komoro”.

Akipokea taarifa hiyo, Balozi Yakubu ameeleza kuridhishwa kwake na huduma ya usafiri wa ndege unaotolewa na ATCL, unaowezesha muunganiko wa safari kati ya Tanzania na Visiwa vya Komoro ambao umeoboreshwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hadi kupelekea kuona uhitaji wa kuanzisha safari za ndege kubwa ya mizigo.
“Mzunguko wa biashara kati ya Tanzania na Visiwa vya Komoro umeongezeka, nasi tuko tayari kuhakikisha nchi zetu mbili zinaimarisha mashirikiano hayo kwa manufaa ya pande zote mbili”, alisema Balozi Yakubu.
Balozi Yakubu amesema kuanza kwa safari za ndege ya mizigo ni ukuaji wa biashara na kuahidi kuwa ofisi yake itaendelea kusaidia shughuli za kiuendeshaji za ATCL ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuifungua nchi kibiashara.
Tangu kuwasili kwa ndege ya kwanza ya ATCL ya mizigo B767-300F mnano Juni 2023, mizigo mikubwa ikiwemo magari, madini, madawa, samani, vipuri na bidhaa zinazoharibika kwa muda mfupi hususan matunda, nyama na mazao ya bahari vimekua vikisafirishwa kutoka na kwenda nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika.
Baadhi ya nchi hizo ni N’Djamena (Chad), Mumbai (India), Dubai (Falme za kiarabu), Nairobi (Kenya), Kinshasha (Kongo), Lusaka (Zambia) na Entebe (Uganda).