×

Majaliwa: Mataifa Madogo Yaungwe Mkono Kiuchumi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Umoja wa Mataifa hauna budi kuyaunga mkono mataifa madogo ambayo hayana uwezo kiuchumi ili yaweze kuboresha mipango yao ya ndani.

Ameyasema hayo jana jioni Jumapili, Septemba 22, 2024, wakati akiwasilisha salamu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kujadili Hatma ya Siku Zijazo (Summit of the Future) ulioanza jana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

Waziri Mkuu ambaye yuko Marekani akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79), amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kuhusu jitihada za Serikali kwenye masuala ya uchumi, ulinzi na mabadiliko ya tabianchi.

Akifafanua kuhusu suala la uchumi, Waziri Mkuu amesema: “Umoja wa Mataifa tunauomba uyaunge mkono mataifa ambayo hayana uwezo ili yaweze kuboresha mipango yao kiuchumi waliyonayo ndani ya nchi yao. Tanzania tumepanga kujenga kesho iliyobora kwa watu wetu kwa kuimarisha kilimo, uwekezaji, viwanda, madini na maliasili.”

“Unapozungumzia ujenzi wa kesho iliyobora kwa watu wako, huwezi kufanikiwa kama hakuna nchi iliyo salama; kwa hiyo ulinzi na usalama ni suala la muhimu na tumeihakikishia jumuiya ya kimataifa kwamba pamoja na ulinzi wa ndani bado ulinzi kwa nchi jirani nao pia wa muhimu,” ameongeza.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya juu wa Wakuu wa Nchi na Serikali ‘Summit of the Future’ uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Mataifa New York nchini Marekani.

Kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi, Waziri Mkuu amesema hivi sasa dunia inashuhudia athari kubwa kwenye baadhi ya nchi kutokana na shughuli za kijamii ikiwemo ukame, mvua nyingi zinazobababisha mafuriko. “Tanzania iko kwenye harakati za kuelimisha wananchi wake kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ili waweze kukaa pamoja na kujadiliana namna ya kukabiliana nayo huku wakiendelea na kazi zao za kiuchumi,” amesisitiza.

Leave a Comment