×

Alvaro Morata Amfokea Meya wa Eneo Analoishi Kisa Kumpost Mitandaoni

Mshambuliaji nyota wa klabu ya AC Milan na nahodha wa timu ya taifa ya Hispania, Álvaro Morata (31) ameonesha kuchukizwa na kitendo cha Meya wa Manispaa ya Corbetta kuweka hadharani taarifa za makazi kuhusu mchezaji huyo.

Mshambuliaji huyo hivi karibuni alifanya uamuzi wa kupanga nyumba mpya katika Manispaa ya Corbetta, sehemu ambayo ni karibu zaidi na ulipo Uwanja wa San Siro unaotumiwa kama uwanja wa nyumbani wa AC Milan ambapo baada ya taarifa za ujio wa Morata katika manispaa hiyo kumfikia Meya wa eneo hilo, Marco Bellarini, meya huyo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram alizichapisha taarifa hizo na kuziweka hadharani hapo jana Jumatano ya Oktoba 2, 2024 kwa kutumia picha ya Morata kisha kuambatanisha na ujumbe wa maandishi uliosomeka;

“Bingwa Álvaro Morata ni mkazi wetu mpya wa Corbetta. Mfungaji wa Hispania, aliyesajiliwa na AC Milan hivi karibuni, anakamilisha uhamisho katika nyumba mpya nzuri katika mji wetu. Wote mnajua mimi ni shabiki mkubwa wa Inter, ila nina furaha kumkaribisha Álvaro Morata katika familia kubwa ya Corbetta”

Kitendo hicho kimeonesha kumchukiza sana mchezaji huyo ambaye leo hii katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram aliandika ujumbe katika ‘Instagram story’ wa kumfokea meya huyo

“Mpendwa Mheshimiwa Meya, asante kwa kukiuka faragha yangu. Kwa bahati nzuri similiki mali yoyote ya thamani. Hazina yangu pekee ni watoto wangu ambao usalama wao umevurugwa na wewe. Nilifikiri kwamba manispaa ya Corbetta inaweza kunihakikishia usiri fulani lakini badala yake najikuta nalazimika kuhama mara moja kutokana na meya kutokuwa na uwezo wa kutumia mitandao ya kijamii na kulinda raia wake.”

Ikumbukwe, mshambuliaji huyo alijiunga na miamba hio ya Italia katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka 2024 kwa ada ya uhamisho iliyogharimu Tsh. 39.6 Billion kwa mkataba wa miaka minne na uwezakano wakuongeza mwaka mmoja kama atahusika katika magoli 20 msimu huu wa 2024-25, ambapo hadi sasa mchezaji huyo akiwa na jezi ya AC Milan amefanikiwa kucheza michezo minne na kufunga magoli mawili.

Leave a Comment