
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kituo cha Daraja B Wilaya ya Chemba, Dodoma leo tarehe 3 Oktoba 2024, ambapo kukamilika kituo hicho kunakwenda kusogeza huduma za kipolisi karibu zaidi na wananchi.
Mhandisi Masauni akiongea baada ya Kukagua na kuweka jiwe la msingi amesema dhamira ya Serikali ni kulisogeza Jeshi la Polisi karibu zaidi na wananchi kupitia sera ya Polisi Jamii na ndio maana kuna askari wa cheo cha nyota moja katika kata zote nchi nzima.

“Serikali ya awamu ya sita inafanya maboresho ya mazingira ya kufanyia kazi Askari wa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya Polisi vipya na vyakisasa, vitendea kazi na stahiki mbalimbali kwa Askari”. Alisema Mhandisi Masauni
Wakati huo huo, Mhandisi Msauni amelitaka Jeshi la Polisi kuendana na maboresho hayo yanayofanywa na Serikali kwa utendaji kazi mzuri unaozingatia weledi na maadili ya kazi zao ili kuakisi jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutatua kero za Wananchi.
Aidha mradi huo umegharimu kiasi cha Tsh Milion 350 mpaka kukamilika kwake ambapo sasa upo katika hatua za umaliziaji.

Katika hatua nyingine Mhandisi Masauni amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Pahi, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ambapo kipekee amefanya harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo Polisi cha Kata hiyo, na kufanikisha kupata kiasi cha Tsh Milioni 18.4, ambapo ujenzi unatarajia kuanza mwezi wa Novemba waka huu.
Mhandisi Masauni yupo kwenye Ziara ya Kikazi Mkoa wa Dodoma, ambapo pia ametembelea na kuunga mkono jitihada za wananchi katika ujenzi wa Shule la Sekondari Mnania, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na kukagua na kuweka Jiwe la msingi la Ujenzi wa nyumba za walimu katika shule ya Sekondari Bolisa, Halmashauri ya Kondoa Mjini.
