
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kufanya mageuzi makubwa ya kuboresha mandhari ya Zanzibar kwa kujenga barabara za juu kutoka Uzi na Ng’ambwa Kaskazini Unguja hadi Charawe – Chwaka, Mkoa wa Kusini Unguja, ili kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa mikoa hiyo.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua soko jipya la ghorofa mbili Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anayoiongoza.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameahidi kurahisisha huduma za usafiri wa umma kwa kuziagiza mamlaka zinazohusika kujenga vituo vikubwa vya mabasi vitakavyoruhusu mwingiliano wa moja kwa moja baina ya masoko ya Kwerekwe, Jumbi, na Chuini, ili kutoa fursa kwa wananchi na wafanyabiashara kunufaika na masoko hayo.

Halikadhalika, Rais Dk.Mwinyi amewaahidi Wazanzibari kuibadili Zanzibar kuwa kituo bora cha biashara cha kimataifa kwa kutoa fursa za mwingiliano wa wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali kuja nchini, kuuza na kununua bidhaa.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Mwinyi amezitaka mamlaka zinazohusika na Soko la Mwanakwerekwe kutowatoza ushuru mkubwa wafanyabiashara wa eneo hilo, akibainisha kuwa fedha zilizotumika kujenga soko hilo hazikutokana na mkopo bali ni kodi za wananchi wenyewe, hivyo Serikali haitegemei chochote kutoka kwa wananchi na wafanyabiashara wa soko hilo isipokuwa kusaidia kuliendesha na kulitunza soko.

Vilevile, Rais Dk. Mwinyi aliwaahidi wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali sokoni hapo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwaongezea mitaji ya biashara zao endapo watajiunga kwa makundi ili kupata mikopo.