×

Benki Kuu ya Tanzania Kuondoa Kwenye Mzunguko Noti za Zamani

Benki Kuu ya Tanzania inatarajia kuanza kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003, na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 858 la tarehe 11 Oktoba 2024.

Taarifa iliyotolewa leo Oktoba 26, 2024 na Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel M. Tutuba imebainisha kuwa zoezi la ubadilishwaji linatarajiwa kuanza tarehe 06 Januari 2025 hadi tarehe 05 Aprili 2025 kupitia Ofisi zote za Benki Kuu na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa.

Aidha, matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania kuanzia tarehe 06 Aprili, 2025 ambapo baada ya tarehe hiyo, mtu yeyote au taasisi yoyote inayomiliki fedha hizo haitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipo popote duniani; na benki zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko.

Kufuatia zoezi hilo Benki Kuu imetoa rai kwa wananchi wote wenye akiba ya noti hizo za zamani, kuzibadilisha au kuziweka amana kwenye benki yoyote ndani ya kipindi kilichotolewa.

Leave a Comment