
Waziri Jafo alitoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam alipotembelea kiwanda hicho na kujionea ujenzi huo unaoendelea na unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
“Nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa na kwa kweli uzalishaji huu ukianza, utakuwa wa aina yake na wenye ubora mkubwa sana hapa nchini kwa hatutakuwa na haja ya kuagiza mabati ra rangi kutoka nje kama tunavyofanya sasa,” allisisitiza.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itaongeza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa vijana wa kitanzania na kusisitiza kuwa yote haya yamewezekana kufuatia mazingira mazuri yaliyowekwa na Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan ili kukuza viwanda na biashara kwa ujumla.
“Kama serikali tunafikiria kuweka utaratibu wa kuzuia uingizaji wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini hususani mabati ili kulinda soko la ndani,” aliwaambia waandishi wa habari na uongozi wa Alaf mara baada ya ziara hiyo na kuongeza kuwa kwa sasa uzalishaji wa mabati wa ndani unakidhi mahitaji ya ndani kwa hivyo hakuna haja ya kuagiza bidhaa hii kutoka nje.
Waziri huyo pia aliipongeza ALAF kwa kusimamia ubora na kuhakikisha watanzania wanapata thamani ya fedha wanazotoa ili kupata bidhaa za kampuni hiyo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited, Ashish Mistry alisema mtambo mpya utahakikisha uzalishaji ni wa hali ya juu zaidi na pia utaendeshwa na vijana wa kitanzania.
“Tayari kuna vijana 30 ambao ni wa Kitanzania kabisa na wameshapata mafunzo ya kina kuhusu uendeshaji huu wa mtambo mpya wa rangi kwa hivyo hatuna haja ya kuleta watu kutoka nje,” alifafanua na kuongeza kuwa nia yao ni kuendelea kuwa namba moja kwani ndio kampuni kongwe ya mabati nchini inayoadhimisha miaka 62 mwaka huu tangu kuanzishwa kwake.
Meneja Masoko wa ALAF Limited, Isamba Kasaka alisema wanatarajia kuanza uzalishani mapema mwakani na kutoa wito kwa watanzania waendelee kuwaunga mkono kwa kutumia bidhaa za kampuni hiyo.
“Mabati ya rangi sasa yatapatikana hapa hapa nchini baada ya mtambo wetu kukamilika kwa hivyo watanzania watarajie mambo mazuri mwakani,” alisema huku akimpongeza waziri na serikali kwa ujumla kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayopamoja na mambo mengine yamesaidia ALAF kutimiza malengo yake.
ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania kwa kutengeneza mabati ya kuezekea nyumba. Ni kampuni iliyoanzishwa mwaka 1960, na inaendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.
ALAF imeunganisha kikamilifu operesheni, si tu kwa kutengeneza mabati, lakini pia kwa kuzalisha vifaa vinavyotumika katika shughuli mbalimbali za uezekaji wa nyumba. ALAF Limited hutengeneza vifaa mbalimbali vya metali kwa matumizi mbalimbali ya uezekaji wa nyumba.