×

Wanawake Wenye Uhitaji Maalum Wapewa Mafunzo ya Kuendesha Bajaj

Dar es Salaam 3 Novemba 2024: Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala, Tabu Shaibu amewashauri wanawake wote kuchangamkia fursa zinazojitokeza ili ziwasaidie kujiinunua kiuchumi na kuepuka kuwa tegemezi.

Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki Jijini katika hafla fupi ya uzinduzi wa Bajaj inayotumia nishati ya umeme wa jua (Solar) ambapo wanawake wanufaika wa mradi wa She drive to Change waliopatiwa mafunzo ya udereva kwa ufadhili wa Ujerumani walikuwa wakihitimu.

“Niwapongeze sana Shirika la Ladies Joint Forum( LJF), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Ujerumani kuweza kuwafundisha wanawake 30 udereva na wote kuwapatia leseni huku mkiangalia namna ya kuwapatia vyombo vya usafiri ili waweze kujiinua kiuchumi, mimi naamini mwanamke ndiye mwangalizi wa familia na akiwezeshwa anaweza kuinua na wengine,” alisema Tabu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Ladie Joint Forum, Francisca Mboya alisema Bajaj hiyo iliyozinduliwa itasaidia kwa kiasi kikubwa wanufaika wa mradi wa She Drive to Change ambapo watajipatia kipato na kuendeleza maisha yao.

Alisema LJF itaendelea kuongeza Bajaj nyingine kupitia fedha mbalimbali watakazochangiwa na wadau.

“She drive to Change ni mradi wa miezi 12 uliolenga kuwezesha na kukuza uhuru wa kiuchumi wa wanawake 30 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 40 katika kata ya Vingunguti Wilaya ya Ilala Jijini, mradi unaozingatia hasa wahanga walionyanyaswa kijinsia, kina mama vijana walemavu na wale wanaolea watoto wenye ulemavu peke yao,” alisema Mboya.

Naye mnufaika wa mradi huo, Oliva Mushi alisema yeye amemudu familia kwa kulipia ada ya shule watoto wake, anajitegemea kwani hapo awali alikuwa anaishi wa ndugu ila tangu amepatiwa leseni anaendesha Bajaj na amewashauri wanawame wengine wasikate tamaa mafanikio kwani hayapatikani kwa siku moja.

Leave a Comment