
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, amewataka wagombea wote ambao hawajaridhishwa na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa waweke pingamizi ndani ya siku 2 kuanzia 08 – 09/11/2024.
Amesema hayo wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu uteuzi wa wagombea katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
“Kama mnavyojua, leo ni siku muhimu ya uteuzi wa wagombea kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Kanuni ya 18 ya Tangazo la Serikali Na. 571, 573, 574, pamoja na Kanuni ya 17 ya Tangazo la Serikali Na. 572 yote ya tarehe 12 Julai 2024.”
“Kanuni hizi zinamtaka Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kufanya uteuzi wa wagombea leo tarehe 8 Novemba, 2024, kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa kumi kamili jioni.
Mara baada ya uteuzi kukamilika, majina ya wagombea wenye sifa na wale ambao hawajakidhi vigezo vya kugombea yatabandikwa hadharani ili umma uweze kuyapata wakiwemo wagombea wenyewe”.Aliongeza Mhe. Mchengerwa.
Ameendelea kueleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni hizo mtu yeyote aliyeomba kuteuliwa kuwa mgombea au mgombea ambaye hakuridhika na uamuzi uliotolewa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, anaweza kuwasilisha pingamizi na kumuomba Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kupitia upya uamuzi uliofanyika ili amteue kuwa mgombea au atengue uteuzi anaoupinga.